Dk. Kafumu akikabidhiwa fomu na Mkurugenzi wa Uchaguzijimbo la Igunga, Magayane Protace. Wengine ni Viongozi wa CCM, Matson Chizi na Neema Adam |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kiliamua kufuta shamrashara za uchukuaji fomu kwa mgombea wake wa ubunge jimbo la Igunga mkoani Tabora, kuomboleza kifo cha mtoto aliyefariki papo hapo baada ya kugongwa na lori.
Mtoto huyo aliyetambuliwa kwa jina la Peter Ezekiel (12) alikufa papo hapo baada ya kugongwa na lori la mizigo wakati akijaribu kukatiza barabara kutoka katika umati wa wananchi waliokuwa wakisubiri msafara wa mgombea Dk. Dalaly Kafumu, eneo la Hani Hani kiasi cha mita 100 kutoka katikati ya mji wa Ingunga.
Dk. Kafumu na msafara wake alikuwa anatokea mjini Singida akiwa na Mratibu wa Kampeni za CCM katika jimbo hilo, Katibu wa NEC ya CCM, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba huku akisubiriwa kwa hamu na umati wa wananchi katika eneo hilo.
Baada ya ajali hiyo polisi wa usalama barabarani walilikamata lori na dereva wake na kulipeleka kituoni, ingawa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora Anthony Ruta hakuwa tayari kuzungumzia hatua zaidi zilizochukuliwa na polisi wa dereva huyo.
Kamanda huyo alisema kwa njia ya simu kwamba hajafahamu kwa kina tukio hilo kwa kuwa hakuwa ofisini kwa muda mrefu kutokana na kuwa kwenye kikao maalum nje ya ofisi.
"Ni tukio la kusikitisha na la kuhuzunisha sana, kwa kuwa mtoto huyu alikuwa miongoni mwa mamia ya wananchi waliokuwa wakimsubiri kwa hamu mgombea wetu basi hakautakuwa na shamra shamra zozote kuanzia sasa" alisema Mwigulu akizungumza na wananchi waliofurika kwenye Ofisi ya CCM wilaya ya Igunga kujua hatma.
"Tunatoa pole sana kwa wazazi na ndugu na jamaa wa mtoto huyu, na CCM inawaomba wanachama na wananchi kwa jumla kushiriki kwa karibu shughuli zote za msiba huu maana ni wetu", alisema Mwigulu.
Mratibu wa Uchaguzi CCM, Matson Chizi aliwataka wana-CCM kutawanyika kwa utaratibu kwenye ofisi hizo bila shamra shamra zozote na kwenda msibani na kwamba utaratibu kuhusu mgombea kuchukua fomu wangejulishwa baadaye.
Hata hivyo mgombea wa CCM alilazimika kwenda kuchukua fomu akisindikizwa na viongozi wachache wa CCM baada ya Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Ingunga, Martha Bayo kuuambia uongozi wa CCM kwamba hakutakuwa na muda wa kutoka kwa kesho (leo) kama ingeamuliwa kuahirisha kuchukua fomu hizo jana.
Mapema baada ya kutokea ajali hiyo, mgombea wa CCM na msafara wake walifika eneo la tukio na kupakia mwili wa marehemu kwenye gari aina ya Pick Up lililokuwa kwenye msafara na kisha mgombea huyo na msafara wake waliupeleka mwili huo kwenye hospitali ya wilaya ya Igunga kuhifadahiwa.
Wakati mgombea huyo wa CCM akichukua fomu zake jana, wagombea wa vyama kadhaa vikiwemo Chadema na CUF wameshachukua na leo Mkurugenzi wa Uchaguzi jimbo la Igunga atakuwa na kikao na viongozi wa vyama kupanga ratiba ya kampeni.
Kulingana na taarifa zilizopo kampeni zinatarajiwa kuanza kutimia vumbi Septemba 7, 2011, ambapo kampeni za CCM zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Ijumaa wiki hii na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269