Breaking News

Your Ad Spot

Oct 10, 2011

STARS YACHEMSHA MORROCO

Marrakech,
Tanzania (Taifa Stars) imefungwa mabao 3-1 na Morocco katika mechi ya mchujo kuwania tiketi ya AFCON 2012 iliyochezwa leo hapa Grand Stadium na kushuhudia na maelfu ya watazamaji kwenye uwanja huo wenye viti 43,000. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji Morocco ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 19 mfungaji akiwa Marouane Chamakh kwa mpira wa kichwa ambao ulidunda kabla ya kumpita kipa Juma Kaseja wa Taifa Stars. Abdi Kassim aliisawazishia Stars dakika ya 40 kwa shuti la nguvu- umbali wa meta 35 lililomshinda kipa Nadir Lamyaghri kufuatia pasi ya Idrisa Rajab.
Mabao mengine ya Morocco ambayo imepata tiketi ya kucheza fainali za AFCON zitakazochezwa mwakani katika nchi za Equatorial Guinea na Gabon yalifungwa dakika ya 68 na Adel Taarabt. Mbark alifuta matumaini ya Stars kupata sare katika mechi hiyo kwa bao lake la tatu alilifunga dakika ya 90 kwa shuti la chini akiwa ndani ya eneo la hatari.
Mwamuzi Bakary Gassema kutoka Gambia aliwaonya kwa kadi za njano Idrisa Rajab, Juma Nyoso, Dan Mrwanda na Mohamed Rajab wa Stars wakati kwa upande wa Morocoo aliyeoneshwa kadi ya njano alikuwa nahodha wa timu hiyo Houcine Kharja.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen aliwataka wachezaji wake wasikate tamaa kutokana na matokeo hayo kwa vile walicheza na timu bora kuliko wao. Alisema hivi sasa wanatakiwa kuelekeza akili kwenye mechi mbili zilizo mbele yao dhidi ya Chad. Mechi hizo za mchujo kwa ajili ya kuingia hatua ya makundi ya mchujo Kanda ya Afrika kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka 2014 zitachezwa Novemba 11 mwaka huu jijini Ndjamena na Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni/Nassoro Cholo, Idrisa Rajab, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Shabani Nditi, Dan Mrwanda, Henry Joseph, Mbwana Samata/John Bocco, Abdi Kassim na Mohamed Rajab/Mrisho Ngasa.
Morocco; Nadir Lamyaghri, Michael Basser, Abdelhamid El Kaoutari, Badri El Kaddouri, Mehdi Benatia, Younes Belhanda, Houcine Kharja, Mbark Boussoufa, Adel Taarabt/Youssef El Arabi, Marouane Chamakh/Said Fettah na Oussama Assaidi/Karim Al Ahmadi.
Taifa Stars inatarajiwa kurejea Dar es Salaam saa 2.30 asubuhi Oktoba 11 mwaka huu kwa ndege ya Qatar Airways.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+212 618185749

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages