Breaking News

Your Ad Spot

Dec 22, 2011

RAIS AMTEUA LUBUVA KUWA MWENYEKITI TUME YATAIFA YA UCHAGUZI

Jaji Mstaafu Damian Lubuva
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Damian Lubuva kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Aidha, Rais Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Hamid Mahmoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Bwana Julius Benedicto Mallaba kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi, Desemba 22, 2011 na Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Phillemon Luhanjo mjini Dar es Salaam imesema kuwa uteuzi huo umeanza tokea Jumatatu, Desemba 19, mwaka huu, 2011.
Kabla ya uteuzi wake, Mheshimiwa Lubuva alikuwa Jaji katika Mahakama ya Rufani Tanzania na baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi.
Mheshimiwa Lubuva anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mheshimiwa Jaji Lewis Makame ambaye mkataba wake wa utumishi wa umma ulifikia mwisho Julai, mwaka huu, 2011.
Naye Mheshimiwa Hamid alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla ya kustaafu kwake na anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mhe Jaji Omari O. Makungu. Mheshimiwa Jaji Makungu aliteuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye akateuliwa kuwa Jaji Mkuu.
Naye Bw. Mallaba, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Sehemu ya Mikataba (Contracts and Treaties) katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bw. Mallaba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bwana Rajabu Kiravu ambaye amemaliza mkataba wake wa utumishi Septemba, mwaka huu, 2011.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages