Breaking News

Your Ad Spot

Dec 9, 2011

WAKUBWA TIMIZENI AHADI ZENU ACHENI VISINGIZIO-AFRIKA

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Mhe. Ombeni Sefue
akizungumza katika mkutano huo.
Na Mwandishi Maalum
New York
Wakati utekelezaji wa  makubaliano ya kimataifa ya kufadhili maendeleo kwa nchi maskini  yakiwa yamekwama, huku washirika wa maendeleo wakijipanga kupunguza misaada yao kwa nchi zinazoendelea. Afrika kwa Upande wake imewataka washirika hao kutimizia ahadi zao za huko nyuma na kuacha  kusingizia mdodoro wa uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika ,Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue amesema, nchi zilizoendelea  zinawajibu wa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano ya Monterrey na Azimio la Doha. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba nchi zinazoendelea na hususani za Afrika zimejitahidi kutimiza  ahadi zake.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,  walikutana katika mkutano  wa Tano wa Kilele ambapo kwa siku mbili,  walijadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu suala zima la  ufadhili wa maendeleo, utekelezaji wake na mwelekeo wa baadaye. Majadiliano yaliyojikita katika  taarifa za  makubaliano ya mikutano ya kimataifa  Monterrey na Azimio la Doha.

“ Afrika kwa upande wake imejitahidi sana  kutimiza  karibu mambo yote iliyoahidi katika mikutano hiyo miwili. Mambo  hayo  tuliyoahidi na ambayo ninapenda kuyarudia tena leo hii, ni  pamoja na kumiliki ajenda zetu za maendeleo, ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani,  sera na mipango  mizuri ya kukuza uchumi, utawala bora , utawala wa sheria, amani na utulivu” akasema Balozi Sefue.

Akasema matokeo ya utekelezaji wa  ahadi hizo ni ya kutia moyo sana. “ tunaamani tungeweza kufanya vizuri zaidi kama tungepata misaada zaidi tuliyoahidiwa kutoka kwa washirika wetu” akasisitiza Balozi Ombeni Sefue.

Katika hotuba yake hiyo ambayo ilipokelewa vizuri na kupongezwa na baadhi wa wajumbe wa mkutano huo, akiwamo mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa. Balozi aliongeza pia kwamba hata kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Afrika imekuwa ikifanya vizuri licha ya vikwazo mbalimbali  vikiwamo  vya mifumo pendelevu  na baguzi ya uchumi wa soko na biashara.

“Afrika tumejitahidi sana,   licha ya kwamba hivi sasa dunia inakabiriwa na mdororo wa uchumi, uchumi wetu kwa baadhi ya nchi unakuwa kwa kiwango kinachoridhisha.  Na ukuaji huu ingawa si mkubwa sana  unatokana na  mahitaji makubwa ya bidhaa kutoka nchi za afrika kwenda katika nchi zinazoinukia kiuchumi” akabainisha mwakilishi huyo wa Tanzania.

Akizungumza utekelezaji wa ahadi  ambazo zimetolewa na  nchi wa hisani kabla  hata ya mdororo wa uchumi na ambazo  hadi sasa bado hazijatekelezwa.

 Balozi Sefue anasema “ wakati kiwango cha misaada kwenda Afrika  kiliongezeka kwa asilimia 4 mwaka 2010, bado kuna changamoto ya  kufikia utekelezaji kamili wa  ahadi za maendeleo zilizotolewa katika mikutano ya kimataifa  ukiwamo ule wa G8.   Tunahitaji kuimarisha  ubora wa kiwango wa misaada hiyo na uhakika wa  upatikanaji wake” anasititiza na kuongeza

“ Mdororo wa uchumi na matatizo ya kifedha yanayozikabilia nchini zilizoendelea kisiwe kisingizio kwenu ( nchi zilizoendelea) cha kuto timiza ahadi zenu   mlizoahidi kuzisaidia nchi zinazoendelea, tumetimiza ya kwetu na nyie timizeni yenu. Tunawashukuru wale wote waliotangaza nia zao za kutekeleza ahadi zao na tunawahimiza wengine kufanya hivyo”.

Aidha Balozi Sefue amewaeleza wajumbe wa mkutano huo ambao pia uliwashirikisha baadhi ya  mawaziri kutoka nchi kadhaa na ulifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro. 

Anasema  nchi nyingi za Afrika  zinafanya jitihada kubwa ya kuimarisha uzalishaji na kuhimili ushindaji katika uuzaji wa bidhaa zake .

“ Nchi za afrika zinataka kufanya biashara miongoni mwao ili kujikomboa na umaskini.  Lakini wakati  misaada ikiongezeka kwa upande wa biashara katika miaka michache ilioyopita, mfumo mzima wa biashara ya  kimataifa  bado si mzuri. Afrika inaendelea kuumia kiuchumi kutokana na  mifumo mibaya  na isiyo sawa ya sheria za biashara” akabainisha.

Akasisitiza kwa  kusema,  kutokana na  ubaguzi katika  mfumo  zima wa biashara ya kimataifa,mchango wa  bara la Afrika katika  biashara ya kimataifa  kwa mwaka  2009  ulikuwa ni asilimia 3.1.

“ Tulitegema mazungumzo ya Doha, yaliyotarajiwa  kukamilisha mwezi disemba mwaka 2005 na ambayo yamekwama tangu mwaka 2008 yangeweza kutoa mwelekeo na matokeo mazuri lakini imekuwa kinyume chake.

Katika hatua nyingine, Balozi Ombeni Sefue, amesema Afrika inahitaji kusaidiwa katika kuweka mikakati na mipango bora ya kuimarisha vyanzo vyake vya mapato ili kufidia kile kinachopunguzwa na wahisani.

“Mdororo wa uchumi umeiadhiri Afrika vibaya sana , na hasa katika uwezo wake wa kukusanya mapato yake ya ndani. Na kwa sababu hiyo tunaomba kusaidiwa katika  kuimarisha uwezo watu wa kitaifa katika  kukusanya mapato ya ndani” akasihi Balozi Sefue kwa niaba  ya  Afrika.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages