Breaking News

Your Ad Spot

Mar 6, 2012

WAANDISHI IRINGA WATUMIA MANDAMANO KUDAI HAKI

Maandamano ya  wandishi wa habari  mkoa  wa  Iringa yamesababisha baadhi ya wananchi  kusitisha  shughuli  zao na  kushiriki maandamano hayo.

Mwandishi wa habari aliyeko Iringa amesema maandamano hayo  yaliyopita  mitaa mbali mbali ya mji  wa Iringa  likiwemo eneo la stendi  kuu ya mabasi  yaendayo mikoni  ambako mwandishi huyo anasema wasafiri   walishuka katika mabasi  walimokuwa kwa ajili ya kuanza  safari na kuungana na  wanahabari hao kwa  kusindikiza kwa muda maandamano  hayo .

Wakitoa maoni yao  juu ya maandamano  hayo  baadhi ya wananchi  wakiwemo Maneno  Mbuma na mzee Said  Sanga  walisema kuwa  hofu ya mkuu  wa mkoa  wa Iringa  kupokea  maandamano hayo   haikupaswa  kuwepo kutokana na utulivu  na hekima  ya hali ya juu  iliyoonyeshwa na  wanahabari hao.

Mbuma alisema  kuwa jamii ya mkoa  wa Iringa haipotayari  kuendelea  kukosa  haki  yao ya msingi ya  kupata habari kwa  ubaguzi  na manyanyaso ya ofisi ya mkuu  wa mkoa  wa Iringa  dhidi ya  wanahabari na  kuwa vyombo  vyote  vya habari  vinapaswa  kupewa haki  sawa ya kuhabarisha  umma juu ya matukio  yanayotokea katika mkoa.

Hivyo  alisema kama kweli  ofisi ya mkuu  wa mkoa  wa Iringa haikuwa na matatizo  hayo ambayo  wanahabari  wameamua  kuyapinga  basi mkuu  wa mkoa  Dkt  Christina  Ishengoma  angekubali  kupokea maandamano hayo ya amani  ila  kukimbia  kupokea maandamano hayo ni  sawa na kuogopa ukweli dhidi ya  ofisi yake.

Akipokea maandamano  hayo ambayo kwa mujibu wa mwandishi wa habari hiyo walikuwa zaidi ya 60 wa  vyombo mbali mbali  mkoani  Iringa  Mwenyekiti  wa Klabu ya Waandishi  wa Habari mkoa  wa Iringa (IPC) ambao  ndio  walidhamini maandamano  hayo,Daud Mwangosi  alisema  kuwa wengi  wamekuwa  na mitazamo  tofauti   juu ya maandamano hayo.

Alisema baadhi ya  watu  wamedhani  wanahabari hao  wanaandamana kwa ajili ya  kutetea kulipwa  posho na  baadhi kuhusisha maandamano hayo  na itikidi  za  kisiasa na  kuwa maandamano  hayo hayakuwa na mitazamo  hiyo kama  wanavyofikiri  bali kupinga manyanyaso dhidi ya  wanahabari na ubaguzi dhidi yao.

Pia  alitaka  wanahabari mkoani  Iringa  kutokubali  kuendelea  kunyamaza  kimya  kwa kile akichokiita ubaguzi unaofanywa na  ofisi ya mkuu  wa mkoa  wa Iringa pamoja na ofisa habari  wa  ofisi  hiyo  Denis Gondwe .

Alisema  kuwa IPC  itaendelea  kuwaunga mkono  wanahabari  katika kupinga  vitendo vyote  vya ukandamizaji  na manyanyaso  kwa wanahabari katika mkoa  wa Iringa  na kuendelea  kuungana na vilabu vya  wanahabari  kute nchini ambavyo havipo tayari  kunyanyaswa na  vyombo  vya umma na  kuyanyima haki  yao ya  kutoa habari ama kupata   habari.

Mwangosi   pia  amewapongeza viongozi  wa  vilabu  vya  wanahabari  mkoa  wa Mbeya, Ruvuma , Arusha na mikoa mingine  ambayo imetoa tamko  la kuunga mkono maandamano  hayo  ya wanahabari  likiwemo   jukwaa la   wahariri  hapa nchini kwa kutoa msimamo  wao  wa  kuunga mkono maandamano hayo ya amani.

Waandishi hao wamesema iwapo mkuu  wa mkoa  wa Iringa Dkt Ishengoma hatajibu madai  yao na kuendelea na msimamo  wake wa  kupuuza madai ya  wanahabari hao  basi  hawatakuwa  tayari  kushirikiana na ofisi yake .

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages