TUZO YA MWANAMICHEZO BORA WA TANZANIA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Jumapili Mei 20, 2012 saa nne asubuhi kitatangaza mdhamini wa Tuzo za Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka 2011.
Mdhamini huyo atatangazwa kwenye mkutano ambao ataufanya Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto pamoja na mdhamini wa tuzo hizo, ambapo mkutano huo utafanyika kwenye mgahawa mpya uitwao City Sports & Lounge uliopo jirani na mnara wa askari makutano ya barabara ya Samora na Azikiwe, Posta Dar es Salaam.
TASWA inachukua fursa hii kuwaalika waandishi wote wa habari za michezo kuhudhuria kwenye mkutano huo ili tuweze kuanza pamoja katika mbio hizi za kuelekea kwenye Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2011.
Tayari Kamati ya Tuzo ishateuliwa na imetangazwa, hivyo baada ya mkutano huo taratibu nyingine zitatangazwa kwa kadri zitakavyokuwa zimekamilishwa na Kamati Maalum ya Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania.
Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan.
KIFO CHA MAFISANGO
TASWA imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiungo wa timu ya Simba ya Dar es Salaam na mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mutesa Mafisango kilichotokea alfajiri ya Alhamisi kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam.
TASWA inatoa pole kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, wachezaji wa timu hiyo, mashabiki na Watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu.
Tunaamini waandishi wa habari za michezo wameguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huo, kwani wakati wa uhai wake marehemu alikuwa na ushirikiano mkubwa na wanahabari na hakuwa mtu mwenye maringo, kiasi cha kushindwa kutoa ushirikiano kwa wenzake.
Tunasema kifo chake ni pigo si kwa Simba na familia yake tu, bali hata kwa timu ya Taifa ya Rwanda na Wanyarwanda wote, ambao pia tunawapa pole kwa msiba huo.
Tunawapa pole wanamichezo wote na kuwaomba wawe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, huku wakiamini waandishi wa habari za michezo tupo nao pamoja katika majonzi hayo na kumuomba Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peoni. Amina.
Kifo cha Mzee Limonga
Tunapenda kuwajulisha waandishi wa habari za michezo wote pamoja na wadau wengine kuwa mtangazaji wa habari za michezo wa Redio Uhuru, Limonga Justine, amefiwa na baba yake mzazi jana Alhamisi asubuhi kwenye hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.
Msiba upo Mbagala kwa Mangaya, Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi. Naomba tuungane naye mwenzetu katika kipindi hiki kigumu kwake na tumfariji kwa kadri tuwezavyo kwa kuondokewa na mzazi wake. Nambari yake ya simu ni 0713-604578.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
18/05/2012.
0713-415346
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269