Breaking News

Your Ad Spot

Jun 18, 2012

BYE WILLY EDWARD OGUNDE

Kifo cha alieyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Ogunde  aliyefariki dunia jana mjini Morogoro kimepokewa kwa mstuko na majozi makubwa na wana tasnia ya habari, na bila shaka na watu wengi ndani na nje ya Tanzania, kutokana na ukweli kwamba kila aliyemfahamu akiwemo Mtayarishaji Mkuu wa Mtandao huu, Bashir Nkoromo, hata sasa anakiri kwamba Ogunde, alikuwa mtu wa watu achilia mbali kuwa mahiri katika kazi yake ya uandishi wa habari.
    Ikitangaza rasmi kifo hicho, Bodi ya Wakurugenzi na wafanyakazi wa Jambo Concepts Ltd inayochapisha gazeti la Jambo Leo na Jarida la Jambo Brand imesema  yafuatayo;-

"Tunasikitika mno kuondokewa na mfanyakazi wetu ambaye alikuwa mchapakazi na mwenye ueledi mkubwa katika tasnia ya uandishi wa habari. Kwa wanaomfahamu Willy watakuwa mashahidi wa hilo tunalosema.
   Hadi sasa hatujapata taarifa rasmi za kidaktari kuhusu kifo chake, lakini taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu zinasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo".

WASIFU
Willy Edward Daniel Ogunde (pichani)  alizaliwa Machi 7, 1974 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
      Alisoma shule ya msingi Mapinduzi mwaka 1983 hadi 1989 kisha elimu ya Sekondari katika shule ya Serengeti mwaka 1990 hadi 1993.Baadaye alijiunga na shule ya Sekondari Musoma kidato cha tano na sita mwaka 1994 na 1995.
       Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya BTL akiwa mwandishi wa gazeti wakati huo likiitwa Majira Jioni.
       Akiwa na kampuni hiyo alipata mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.
      Mwaka 1998 alihamishwa kitendo kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar Leo na kuwa mwandishi wa habari wa hazeti hilo lakini pia akishikilia nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.
      Alifanikiwa kuaminika na kutokana na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
      Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti hilo .
       Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).
       Amesafiri nchi mbalimbali duniani katika kuripoti habari za michezo na burudani ikiwemo Afrika Kusini mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.
        Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 Kenya, Senegal na Uingereza kuripoti habari za michgezo kupitia Super Sport.
       Mei mwaka huu alisafiri kwenda nchini Uturuki kwenye kongamano la wadau wa masuala ya mawasiliano ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
       Nje ya kazi ya uandishi wa habari mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.
      Miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na Kampuni ya New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa Mhariri Msaidizi wa gazeti la Bingwa.
     Hatimaye mwaka 2008 alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na kujiunga na Kampuni ya ZK.
     Alijiunga na gazeti la Jambo Leo mwaka 2010 akiwa Mhariri wa Habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti ilipomkuta alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.
     Taarifa hii imetolewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Ltd.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages