Breaking News

Your Ad Spot

Jun 18, 2012

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA MHARIRI MKUU WA JAMBO LEO


Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JamboLeo, Ndugu Willy Edward Ogunde kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, Juni 17, 2012  mjini Morogoro.
Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema katika salamu zake za rambirambi, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana ingawa tayari alikuwa amekwishakutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari kutokana na umakini wake, uzingatiaji  wa weledi kikamilifu na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, huko Morogoro ambako alikuwa amekwenda kikazi. Ndugu Willy Edward Ogunde amepoteza maisha akiwa bado kijana sana hata kama ni kweli katika muda mfupi wa maisha ametokea kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari kwa mchango wake wa kudumisha weledi na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mheshimiwa Waziri salamu za dhati ya moyo wangu za rambirambi kuomboleza kifo cha kijana huyu wetu na mwanataaluma wako. Aidha, kupitia kwako nakuomba uniwasilishie salamu zangu kwa wanataaluma wote wa tasnia ya habari nchini kwa kuondokewa na mwenzao. Lakini zaidi, nakuomba unifikishe salamu zangu nyingi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Willy Edward Ogunde.”
“Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu pia. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kufiwa na mpendwa wao. Nawaombea subira na uvulivu. Aidha, wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Will Edward Ogunde. Amina,” amesisitiza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages