Breaking News

Your Ad Spot

Sep 7, 2012

KAJUBI MUKAJANGA RAIS MPYA WA CHAMA CHA MABARAZA YA HABARI DUNIANI (WAPC).


Katibu Mtendaji wa  Baraza la Habari Tanzania, (MCT), Kajubi Mukajanga (pichani) amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mabaraza ya Habari Duniani  (WAPC).

Kajubi  ambaye alikuwa Kaimu Rais wa chama hicho,  alichaguliwa na Kamati ya Utandaji ya WAPC katika mkutano wake uliofanyika katika ukumbi ulioko kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Ahamisi Septemba 6, 2012.

Alishika wadhifa wa Kaimu Rais wa WAPC  baada aliyekuwa Rais wake Jaji  Dr. G.N. Ray  wa  India kustaafu uenyekiti wa Baraza la Habari la India na hivyo kukosa sifa ya kuendelea kushika wadhifa wa uongozi katika chama hicho cha dunia.

Sharti muhimu la kuwa kiongozi katika WAPC ni  muhusika kuwa na nafasi ya uongozi katika Baraza la Habari la nchi yake.  

Katika uchaguzi  huo, Chris Conybeare wa  Hawaii, Marekani alishikilia wadhifa wake wa Katibu Mkuu  wakati  Kishor Shrastha  kutoka Nepal   alichaguliwa  kuwa mmoja wa Makamu wa Rais wa chama hicho.

Makamu  mwingine wa Rais  aliyechakuliwa na mkutano huo ni Sule Aker kutoka Cyprus Kaskazini ingawa mwenyewe hakuwepo. Dk. Tamer Atebarut wa Uturuki  alichaguliwa tena kuwa Mweka Hazina.

Hii  ni mara ya pili  WAPC  kufanya mkutano mkutano Tanzania. Mkutano wa kwanza  ulifanyika 2004 Bagamoyo.

Wote waliochaguliwa kushika nyadhifa  mbalimbali kwenye WAPC watashika nafasi  hizo kwa  kipindi cha miaka mitatu.  Katika mkutnao huo,  Pakistan  ilikubaliwa kujiunga  kuwa mwanachama wa WAPC .

Mkutano huo wa WAPC unofanyika mara moja kila mwaka  uliteua kamati mbili  za kushughulikia mikakati  na kupendekeza  hatua za kukifanya chama hicho kuwa endelevu  na  kupendekeza marekebisho ya katika yake.

Kamati hizo ambazo kila moja ina wajumbe watatu wakimjumisha Katibui Mkuu Conybeare  zimepewa muda wa miezi mitatu kukamilisha majukumu yake.

Katika mkutano huo pia nchi wanachama ziliwasilisha taarifa kuhusu hali ya vyombo vya habari ikiwemo uhuru wa habari na wa kujieleza na mafanikio na matatizo katika vyombo vya habari katika nchi zao.
Mkutano wa unaofuata wa WAPC umepangwa kufanyika nchini Kenya.

Katibu Mtendaji wa  Baraza la Habari la Kenya Dk.      Haron Mwangi  alieleza   utayari wa nchi yake  kuwa mwenyeji wa mkautano huo Mei 3, 2013 ili kwenda pamoja na maadhimishio ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Habari  inayoadhimisha  kila Mei 3.

Nchi zilizoshiriki  mkutano  wa Mikumi ni Zimbabwe, Turkey, Nepal, Marekani, Pakistan, India, Uganda, Kenya, North Cyprus, Malawi,  na wenyeji Tanzania. Mwakilishi wa Shelisheli  alihudhuria mkutano huo kama mgeni mwangalizi.

Katibu Mkuu wa WAPC , Conybeare, aliuelezea mkutnao huo kuwa ni wa mafanikio na kuongeza kuwa chama hicho sasa  kinalenga kujumuisha nchi zote wanachama ambazo zinaonakena uanachama wake hauko hai.

Alisema pia  kuwa ni vizuri kwamba Pakistan  imejiunga na  WAPC  na  Shelisheli iko katika mchakato wa kujiunga na chama hicho.

Wakiwa nchini  wajumbe hao wa Kamati ya Utendaji ya  WAPC  walikutana na  Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenelle Mkangara mjini Dar es Salaam Septemba 4, 2012 kabla ya  kwenda  Zanzibar  walikokutana na Makamu wa pili wa Rais Septemba 5, Balozi Seif Ali Idd. Baadaye siku hiyo walitembelea mashamba ya  viungo  nje kidogo ya mji wa  Zanzibar. PICHA ZAIDI BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages