Breaking News

Your Ad Spot

Sep 7, 2012

RAIS KIKWETE AWASILI UGANDA

KAMPALA, UGANDA
RAIS Jakaya Kikwete amewasili mjini Kampala, Uganda, jioni hii, kuhudhuria mkutano maalumu wa  Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), ambao utajadili hali ya usalama ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mkutano huo ni mwendelezo wa mwingine uliokwisha kufanyika kuzungumzia hali ya usalama katika eneo hilo, hususan  Goma, ambako waasi wa kundi la M23 wamekuwa wakipambana na majeshi ya serikali ya DRC kwa muda mrefu, huku wakishikilia  baadhi ya maeneo.

Rais Joseph Kabila wa DRC na Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kuwa ni kikwazo cha amani nchini DRC kwa kusaidia waasi wa kundi hilo, linaloongozwa na Jenerali muasi Bosco Ntaganda.

Kwa mara kadhaa Rais Kabila amekuwa akiitaka Rwanda kukoma kuingilia mambo ya ndani ya DRC na aliuomba Umoja wa Afrika (AU) kuharakisha mpango wa kutuma majeshi ya kulinda amani katika eneo la Goma.

Hata hivyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda, amekanusha tuhuma hizo akisema ripoti ya Umoja wa Mataifa haikufanyiwa utafiti wa kutosha kuhusu suala hilo.

Kutokana na hilo,  Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliitisha mkutano mwezi uliopita uliojadili hali ya usalama Mashariki mwa DRC.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages