NA MWANDISHI MAALUM NEW YORK
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema, vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo wakati wakujifungua havipaswi kutokea na havikubaliki.
Na kwa sababu hiyo, anasema juhudi zaidi zinahitajika katika kubabiliana na hali hiyo na hasa ikizingatia kwamba sababu zinazosabisha kutokea kwa vifo hivyo zinazuilika.
“ Vifo vya wanawake wajawazito havikubaliki” akasema na kuongeza “ na ndiyo kwasababu tunahitaji kuongeza juhudi zaidi kuokoa maisha ya wanawake, kwa sababu si haki na si jambo jema kwa mwanamke kufa wakati wa kujifungua , si haki afe wakati akimleta kiumbe mwingine duniani, na cha kusikitisha zaidi wanakufa kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika”. Akasisitiza Rais Kikwete.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa ubunifu wa uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto katika maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani kwa urahisi nchini Tanzania.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika mbele ya waandishi wa habari siku ya jumanne hapa Makao Uakuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Rais Jakaya kikwete na wafadhili wakuu wa mpango huo ambao ni Meya wa Jiji la New York na philanthropist Michael Bloomberg na Dkt. Helen Agerup, Mkuu wa Mfuko wa H&B Agerup.
Wafadhili hao wawili wametoa dola za kimarekani milioni 15 kufadhili huduma za uboreshaji wa vituo vya afya, na mafunzo ya huduma za upasuaji wa dhararu kwa waganga, wakunga na manesi lengo likiwa ni kuokoa maisha ya wanawake wanapojifungua na kupunguza umbali wa kuifuata huduma hiyo.
Rais Kikwete amesema kwamba, uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto na afya kwa ujumla ni moja ya vipa umbele vyake muhimu na ni jambo lililo ndani ya moyo wake.
“Tumefanya mengi na tunaendelea kufanya, lakini tunahitaji kuongeza kasi ya juhudi hizi, uboreshaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto ni kupaumbele changu ni jambo lililo moyoni mwangu na tunapopata wafadhilli kama nyinyi kuchangia juhudi zetu tunafarijika zaidi na kutiwa moyo na tunawashukuru” akasema Rais.
Naye katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupigania nakutetea haki za wanawake na watoto, amesisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi kuokoa maisha ya wanawake na watoto kwa kuboresha huduma zao.
“Tunahitaji marais, mameya ,wanaharakatiwa kuboresha huduma za afya na wafanyakazi wa afya hadi ngazi ya chini kabisa. Leo tunashuhudia matokeo ya ushirikiano huu ambapo kwa ushirikiano wa viongozi watatu tumeweza katika kipindi cha miaka miwili kupunguza kwa asilimia kubwa vifo vya wanawake wajawazito katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Morogoro na Pwani ambako mpango huu wa ubunifu umekuwa ukitekelezwa” akabainisha Ban ki Moon
Aidha Ban Ki Moon amemuelezea Rais Jakaya kikwete kama mmoja wa viongozi wa kwanza duniani kuungua mkono mkakati wa Kimataifa kuhusu Afya ya mama wajawazito na watoto, mpango uliozinduliwa mwaka 2010 ambapo kiasi cha dola milioni 400 zitaelekezwa katika uboreshaiji wa huduma hizo. Na ni mpango unaokwenda sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Millenia ( MDGs).
Kwa upande wake Meya na philanthropies Michael Bloomberg akizungumza kwenye uzinduzi huo anasema aliamua kuichagua Tanzania kufadhili uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na kuvutiwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi.
“Mwaka 2006 niliamua kuwekeza Tanzania kwa kubuni mpango huu wa kuboresha huduma ya dharura ya uzazi hasa katika maeneo ambayo hayafikiki na hakuna huduma za afya. Niliamua hivi kwa sababu nilivutiwa sana na juhudi za Rais Kikwete, ni kiongozi makini, imara na ambaye amekuwa mstari wa mbele katika suala hili, Tanzania inabahati ya kuwa na kiongozi kama huyo” akasisitiza
Na kuongeza kwamba mpango wake huo ambao amesema ni wa aina yake na wa kwanza kufanyika na umeanza katika maeneo machache kwa lengo la kuona maendeleo na mafaniko yake ili baadaye uweze kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi.
Naye Dkt. Helen Agerup, yeye amesema ameamua kuugana na Meya Bloomberg kufadhili mpango huo kutokana kuvutiwa na kazi nzuri inayofanywa na Meya na kubwa zaidi baada ya kujionea kwa macho yake kile ambacho kimekuwa kikifanyika nchini Tanzania.
“Nilikwenda Tanzania mimi na binti yangu na mume wangu, tukajionea kazi nzuri ya ubunifu huu na namna ilivyoweza kuokoka maisha ya wanawake wajawazito. Tumeamua kuwekeza kwa sababu kile tulichokiona Tanzania kimekidhi malengo ya mfuko wetu, kwa sababu tunahitaji kufanya jambo ambalo matokeo yanapimika, yanaonekana na yanazaa matunda na haya yote tumeyashuhudia Tanzania”. Akabainisha Dkt. Hellen
Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na onesho la video fupi iliyoonyesha kile kilichokuwa kikifanyika nchini Tanzania, kwa maana ya uokoaji wa vifo vya wanawake wajawazito kwa utoaji wa huduma za dharura za upasuaji baada ya waganga na wakunga kupewa mafunzo ya upasuaji wa dharura.
Aidha video hiyo imeonyesha wanawake wakipoteza maisha aidha kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua au kupata maambukizo wakati wa kijifungua. Lakini imeonyesha pia jinsi ya wataalamu hao wakitoa huduma hiyo kwa uhodari na uadilifu mkubwa na nyuso zao zikiwa zimejaa faraja hasa baada ya kupewa mafunzo kupitia mpango huo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269