.

TUME YA AJALI YA MELI YA SKAGIT YATOKA LEO

Nov 19, 2012


ZANZIBAR, TANZANIA
Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuchunguza ajali ya meli ya MV. Skagit iliyotokea tarehe 18.7.2012 ilipokuwa ikitokea Dare s Salaam kwenda Zanzibar imependekeza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu watu saba kwa makosa mbali mbali yaliyochangia kutokea kwa ajali hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini na watendaji wa Taasisi zinazosimamia suala hilo na kuepusha ajali za mara kwa mara.

Akitoa taarifa ya Tume hiyo kwa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Mnazimmoja, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee amewataja watu waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kisheria ni mmiliki wa MV.Skagit ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa  Kampuni ya Seagull Sea Transport Said Abdul-rahman Juma, Nahodha wa meli hiyo Makame Mussa Makame na Meneja wa Kampuni hiyo tawi la Dar es salaam Omar Hassan Mkonje.

Amesema kutokana na matendo yao ya kuwa karibu mno na sababu zilizopelekea kutokea kwa ajali hiyo, Tume imependekeza watu hao washtakiwe kwa kosa la kusababisha vifo kutokana na uzembe.

Mmiliki wa kampuni hiyo amefanya kosa la  kufanya biashara ya usafiri wa baharini kwa kutumia chombo ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria na kutumia chombo ambacho hakikutimiza masharti ya ukaguzi kwa mujibu wa sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006, kumuajiri nahodha bila ya kuwa na cheti cha umahiri cha daraja la tano  na kuruhusu meli kupakia idadi kubwa ya abiria kinyume na uwezo wake.

Abdulhamid amesema taarifa hiyo imesema Nahodha Makame Mussa ametenda kosa la kuendesha meli akiwa hana cheti, kushindwa kuwaandaa abiria  kujiokoa wala kutoa taarifa ya dharura, kuendesha meli hali ya kuwa si salama na kuruhusu kupakia abiria 431 badala ya 250 iliyoainishwa kwenye cheti cha abiria.

Watu  waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni  aliekuwa Mkaguzi wa meli na Kaimu Mrajisi wa meli kutoka Mamlaka ya usafiri wa baharini Zanzibar Juma Seif Juma, Mkaguzi wa kujitegemea Capt. Saad Shafi Adam na Maafisa wa usalama wa bandari ya Dar es Salaam Johari Mikidadi  Ndumbati na Peter Ndimbwa Mwasi kwa kushindwa kudhibiti uingizaji wa abiria katika meli ya MV. Skagit siku iliyopata ajali ikiwa ni kinyume na majukumu yao ya kazi.

Taarifa hiyo imetoa mapendekezo ya kuimarisha Sheria na kanuni za usafiri wa baharini namba 5 ya 2006 kwa kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu ikiwemo kuweka utaratibu wa kisheria utakaowalazimisha wafanyabiashara wa usafiri wa baharini kuwa na utaratibu wa kuuza tiket za safari pamoja na kutengeneza urodha ya wasafiri kwa njia ya electroniki na kuweka utaratibu wa kisheria unaowalazimisha uongozi wa kampuni unaoendesha biashara ya usafiri wa baharini kuwa na taaluma ya masuala ya usafiri wa baharini.

Aidha Abdulhamid amesema Tume hiyo imependekeza Kampuni kuwalipa fidia abiria wote waliokuwemo ndani ya meli.  Kwa  waliofariki walipwe thamani ya kiwango cha mshahara wa chini cha muda wa miezi 80 na walionusurika na kupata ulemavu walipwe asilima 75 ya kiwango cha waliofariki na watu wengine walionusurika bila ya kupata majeraha yoyote walipwe asilimia 50 ya kiwango   walicholipwa waliofariki.

Katika ajali hiyo watu 81 wakiwemo raia watatu wa kigeni walifariki na maiti zao zilipatikana na kuzikwa,  212 walipotea na 154 waliokolewa wakiwa hai wakiwemo raia 15 wa kigeni.

Katibu Mkuu Kiongozi amesema Tume imeeleza sababu za kutokea ajali hiyo kuwa ni upepo mkali, muundo wa meli ilioruhusu abiria wengi kukaa juu, mwendo wa kasi, nahodha kukosa ujuzi na umahiri na abiria kuwa wengi kupita kiwango chake.

Amesmea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekubaliana na mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10 chini ya mwenyekiti wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Abdulhakim Ameir Issa.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช