Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea kustushwa kwake na tukio la kikatili alilofanyiwa kiongozi wa kidini wa Kanisa katoliki Padri Ambrose Mkenda kupigwa risasi usiku wa Disemba 25 kuamkia 26 mwaka huu mjini Zanzibar.
Taarifa ya Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar wa Idara ya ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu imesema leo kwamba mfululizo wa vitendo hivyo vya kinyama na kiharamia kunakofanywa na watu wasiojulikana kimsingi hakuzingatii thamani ya utu na ubinadamu, ni ukiukaji wa misingi ya kiungwana, ustaarabu na upendo.
"Tukio hili na lile la kuchomwa moto kwa makanisa, kumwagiwa tindikali kiongozi wa kiislam Sheikh Fadhil Soraga miezi mitatu iliopita na Padri Mkenda kupigwa risasi, kunaweza kuipunguzia Zanzibar fahari na sifa zake njema", amesema Warid.
Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar amesema kwa karne nyingi Waislam, Wakristu na wenye dini mbalimbali wamekuwa wakiishi kwa umoja, maelewano kinyume na hali inavyojitokeza sasa visiwani hapa.
Waride alisema matukio hayo yanazidi kusikitisha na kutoipa heko Zanzibar huku yakizidi kuhuzunisha na kwamba CCM inaamini kuwa Zanzibar na Tanzania si nchi za kidini, kila mtu anafuata imani anayoitaka bila kuingiliwa au kubughdhiwa.
"Uhhuru wa kuabudi ni haki ya kikatiba katika katiba zote mbili za Tanzania na Zanzibar hivyo chama chake kinawalaani wale wenye mtazamo wa kuona imani zao ndizo thabit kuliko za wengine". alisema Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Zanzibar.
Msemaji huyo wa CCM Zanzibar alisema licha ya kukiita kitendo hicho ni cha kinyama na kihalifu amesema pia kinaijengea jamii hofu na wasiwasi huku kikilenga kuleta mgawanyiko wa kijamii usio na ulazima.
Alisema uharamia, uhalifu na ubaguzi wowote wa kidini hauwezi kuipa tija Zanzibar na badala yake kutaliviza jina lake zuri lililotuka miaka kwa mika.
Waride aliviomba vyombo vya dola kufanya kila linalowezekana na kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mikono ya sheria.
Alisema Chama Cha Mapinduizi kinamtakia nafuu kwa Mungu Padri Mkwenda ili apone haraka na kuwataka wananchi kuwa wastahamilivu huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269