Na Mwandishi Maalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,
ametaka kuwapo kwa msukumo mpya wenye lengo la kujenga jamii inayothamini
utofauti baina ya watu na
ushirikishwaji.
Ban Ki Moon ameyasema
hayo katika k salamu zake wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu.
Maadhisho hayo hufanyika kila desemba tatu.
Mkuu huyo wa Umoja wa
Mataifa ameeleza kuwa, kwa kutambua
nafasi na mchango wa watu wenye ulemavu
katika sekta mbalimbali, ndiyo maana Umoja wa Mataifa umeandaa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali, mkutano ambao utajadili kwa kina masuala ya
watu wenye ulemavu na maendeleo.
“Maadhamisho haya ya leo “. Akasema Ban Ki Moon,
“ Ni mwanzo wa maandalizi ya mkutano huo wa kilele kwa lengo hasa la kuchochea na kuhakikisha kwamba haki, mahitaji na
mchango wa watu wenye ulemavu vinazingatiwa kwa ukamilifu.
Mkutano huo utafanyika Septemba 23 mwaka 2013 ikiwa ni sehemu ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la 68 la Umoja wa
Mataifa. kufanyika kwake kunatokana na
mchango na msukumo mkubwa uliofanywa
na Balozi za Tanzania na Ufilipioo
katika Umoja wa Mataifa wa kuandaa na kusimamia majadiliano yaliyozaa maazimio
mbalimbali ambayo hatimaye yalijenga ushawishi mkubwa wa kuwa na mkutano huo
katika ngazi ya viongozi wakuu wa nchi na serikali.
Maazimio hayo
likiwamo lililopitishwa hivi karibuni, yanahimiza pamoja na mambo
mengine, ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli na maamuzi
yanayohusu masuala ya maendeleo ikiwamo utekelezaji wa malengo ya
maendeleo ya millennia.
Aidha maamizio hayo yanazihimiza serikali na taasisi
za kimataifa kuwa na mipango madhubuti
na endelevu ya ukusanyaji wa raslimali zitakazohakikisha ushiriki wa kundi hilo la jamii na
halikadhalika maazimio hayo yanaisisitiza pia haja na umuhimu wa kuwa na taarifa na takwimu sahihi za watu
wenye ulemavu.
Katika maadhimisho yaliyofanyika hapa Makao Makuu yakiambatana pia na mijadala mbalimbali, Ban
Ki Moon anasema watu wenye ulemavu wana
mchango mkubwa katika jamii. Na kwamba wanaweza kufanya vizuri zaidi ikiwa
vikwazo vinavyokwamisha ushiriki wao vitaondolewa.
Aidha Ban Ki moon
ameeleza kwamba changamoto kubwa
ni katika utoaji wa fursa sawa na ukidhi
wa mahitajio ya msingi ya watu wenye
ulemavu.
“ kwa umoja wetu lazima tuhakikishe kwamba
tunajitahidi kutekeleza malengo ya
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wenye Ulemavu. Kuondoa ubaguzi na kutoshirikishwa, na kujenga
jamii ambayo inathamini na kuhimiza ushirikishwaji” akasema Ban Ki Moon.
Inakadiriwa kwamba watu bilioni moja sawa na asilimi 15 ya
idadi ya watu wote duniani
wanaishi na aina moja ama nyingine ya ulemavu.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukiadhimisha siku ya
kimataifa ya watu wenye ulemavu tangu mwaka 1992, na mwaka
2007 ulipitishwa Mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na ukaanza kufanya kazi mwaka 2008.
Mkataba huo pamoja na mambo mengine unatambua
vikwazo vinavyowakabili watu wenye
ulemavu kwa sababu tu ya ulemavu wao,
na kwa sababu hiyo Mkataba unatamka kwamba watu wenye ulemavu wana haki ya msingi
ya kupata elimu jumuishi.
Hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu nchi 126 sawa na theluthi mbili ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa
zilikuwa zimeuridhia Mkataba huo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269