Breaking News

Your Ad Spot

Feb 8, 2013

JK AOMBOLEZA KIFO CHA ASKOFU MSTAAFU WA KANISA KATOLIKI JIMBO LA MOSHI


DAR ES SALAAM, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kuomboleza kifo cha Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo la Moshi.

Askofu Msarikie aliaga dunia jana, Alhamisi, Februari 7,2013 katika hospitali moja ya mjini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 82.

Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi kwa Rais huyo wa TEC amesema: “Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia jana mjini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anapata matibabu hospitalini.”

Amesema Rais Kikwete: “Askofu Msarikie ambaye alistaafu rasmi mwaka 2007 baada ya kuliongoza Jimbo la Moshi kwa miaka 22, atakumbukwa kwa mengi. Alikuwa kiongozi hodari wa kiroho. Alikuwa pia mwalimu mwenye sifa za kutukuka. Askofu alitoa mchango mkubwa katika elimu na mchango wake katika maendeleo ya sekta hiyo hautasahahulika kamwe. Alikuwa mkereketwa wa elimu na alichangia sana kuinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Kilimanjaro.”

“Kwa niaba ya serikali ninayoiongoza na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Baba Askofu Ngalalekumtwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Baba Askofu Msarikie. Aidha, nakusihi upokee salamu zangu za pole nyingi kwa viongozi wote na waumini wa Kanisa Katoliki katika Jimbo la Moshi na Tanzania nzima kwa kuondokewa na kiongozi wao, askofu wao na mwalimu wao,” amesema Rais Kikwete.

“Baba Askofu Ngalalekumtwa, naungana nawe, viongozi wenzake na waumini wote wa Kanisa Katoliki Tanzania kuomboleza msiba huu mkubwa. Msiba huu ni wetu sote na machungu ni yetu sote. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema poponi roho ya Marehemu Askofu Amedeus Msarikie. Amen.” alimakiza.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages