PWANI, Tanzania
Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, mama Salma Kikwete, amekabidhi msaada wa vifaa vya tiba na dawa wenye thamani ya shilingi Mil 20, kwenye Kituo cha Afya cha Nyamsati, mkoani Pwani.
Msaada huo umetolewana Mfuko wa Huduma za Jamii wa Vodacom Tanzania (Vodacom Foundation) na hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo, katika Kituo cha Afya cha Nyamsati mkoani hapa, ambapo pamoja na mambo mengine, mama Kikwete ameishukuru Vodacom Foundation kwa msaada huo, nakutoa rai kwa wadau wengine kujitokeza na kuunganisha Nguvu katika kukabiliana na matatizo ya kijamii,hasa eneo la afya ya mama na mtoto.
"Idadi ya vifo vya mama na mtoto, mapambano dhidi ya Malaria na UKIMWI, chanjo kwa watoto ikiwemo ya ugonjwa wa Nimonia, mimba kwawanafunzi wa kike pamoja na kuwawezesha wajasiriamaliwa kike ni mambo muhimu ambayo jamii inapaswa kuyatazama kama changamoto na kuangalia namna ya kukabiliana nayo," amesema.
Mama Kikwete amesema upungufu wadawa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini bado ni changamoto, na kwamba msaada uliotolewa utasaidia kuunga mkono jitihada za Serikali zenye lengo la kuleta ustawi wa huduma za Afya kwa manufaa ya watu wa Nyamsati na mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Akipokea msaada huo, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Nyamsati wilaya ya rufiji mkoa wa pwani Bw.Haruna Mhina alisema Kituo hicho cha afya ambacho kinahudumia wastani ya wagonjwa 2000 kwa mwezi kinakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa madawa na vifaa tiba lakini kupitia msaada huo, kwa kiasi kikubwa utasaidia kutatua ukubwa watatizo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Vodacom,Bw. Yessaya Mwakifulefule, amesema kuwa mfuko huo siku zote umekuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi na vituo kadhaa vya afya nchini katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini kupitia misaada mbalimbali wanayoitoa.
"Azma ya Vodacom nikuhakikisha tunaifikia jamii na kushirikiana nayo katika kukabiliana na changamoto zinazoizunguka kwenye maeneo yote,hususani afya na elimu, na tutaendelea kuisaidia Nyamsati kadiri itakavyowezekana ili kuleta ustawi mzuri kwa afya ya watu wake," amesema Mwakifulefule.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269