Breaking News

Your Ad Spot

Mar 28, 2013

CHINA KUSAIDIA NYANJA ZA BIASHARA, UWEKEZAJI NA UJENZI WA MIUNDOMBINU


Rais wa China Xi Jinping akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere hivi karibuni ambapo serikali yake imeahidi kuisaidia Tanzania katika nyanja za biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundo mbinu, kilimo, mawasiliano na kukuza uwekezaji  katika usafirishaji.

Na Eleuteri Mangi- Maelezo
Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano baina yake na serikali ya Tanzania hasa katika nyanja za biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundo mbinu, kilimo, mawasiliano na kukuza uwekezaji  katika usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam leo, Mshauri wa Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Liu Dong alisema, katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania itaendelea kunufaika na uboreshaji wa upanuzi wa mawasiliano ya kijamii ikiwemo elimu, Utamaduni, teknolojia, afya, utalii na habari.
Akifafanua  hayo  Liu Dong  alionyesha mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa  ni pamoja na kuthaminiwa kwa urafiki wa jadi uliopo kati ya Tanzania na China kupitia Balozi zinazoendelea kufanya kazi pande zote mbili. Aliongeza kuwa hayo ni matunda ya mahusiano mazuri ya kisiasa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Aliendelea kufafanua kuwa manufaa na  maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania kutoka Jamhuri ya Watu wa China kuwa ni pamoja na  kipaumbele cha kuingiza bidhaa nchini humo na kupewa msamaha wa kodi kwa asilimia 95 ambayo ndiyo kiini cha kuimarisha uchumi wa nchi.
Mshauri huyo wa Utamaduni alisisitiza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China umeongezeka licha ya kukabiliwa na mdororo wa kiuchumi wa kimataifa na kuwa uwekezaji wa China kwa Tanzania umepata nafasi ya pili miongoni mwa nchi zote.
“Ninaona fahari kuwa Mshauri wa Utamaduni wa Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusukuma mbele na kushuhudia upanuaji na utekelezaji wa ushirikiano katika fani zote na Tanzania”, alisema Liu Dong.
Aidha, Rais Jinping alipokuwa akihutubia wakati wa ziara yake aliahidi kuwa Tanzania na China zitakuwa marafiki  waaminifu milele.  
Ni siku ya tatu baada ya ujio wa Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu China kuitembelea Tanzania na kuacha mafanikio ya kihistoria   kwa watanzania katika ziara yake ya Kiserikali tangu kuapishwa kwake kuiongoza nchi hiyo.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwenye ziara ya Rais Jinping  na kuonyesha kuwa mahusiano ya China na Afrika na hasa Tanzania yametiwa maanani na imeendeleza ushirikiano na urafiki wa jadi uliopo baina ya nchi hizo ulioasisiwa na wasisi wa mataifa hayo rafiki.
Kabla ya kuitembelea Tanzania Rais alitembelea Urusi, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuhudhuria mkutano wa tano wa viongozi wa kundi la nchi zinazokua kwa haraka duniani yaani Brazil, Rasia India, China na Afrika Kusini (BRICS) uliofanyika Durban Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages