Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Hassan Wakasubi kuomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe na mwanachama mahiriri wa CCM, Mama Mosi Tambwe.
Mama Mosi Tambwe ambaye katika maisha yake alishikilia nafasi za uongozi ndani ya Chama na kuwa mbunge kwa kipindi kirefu aliaga dunia usiku wa kuamkia leo, Alhamisi, Machi 7, 2013 nyumbani kwake mjini Tabora.
Katika salamu zake, Mheshimiwa Rais amemwambia Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tabora: “ Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Mama Mosi Tambwe ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia usiku wa kuamkia leo.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nilimjua Marehemu Mosi Tambwe kwa miaka mingi katika nafasi mbali za uongozi ukiwemo ubunge. Alikuwa mtumishi mwadilifu na mwaminifu wa wananchi na mwakilishi mahiri wa wananchi wa Mkoa wa Tabora na Tanzania kwa jumla.Hakuna shaka kuwa nchi yetu imempoteza mzalendo wa kweli kweli na chama cheti kimepoteza mwanachama hodari sana.”
“Nakutumia Mheshimiwa Hassan Wakasubi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wea Tabora salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mama Mosi Tambwe. Nakupa pole na msiba huu mkubwa na kupitia kwako nawatumia wanachama wote wa CCM na wananchi wa Mkoa wa Tabora kwa jumla pole zangu nyingi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Aidha, nakuomba unifikishie salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa familia ya Marehemu Mosi Tambwe ambayo imeondokewa na kiongozi na mpendwa wao. Wajulishe kuwa niko nao katika kipindi hiki kigumu. Naelewa machungu yao na naungana nao katika kuomboleza kifo cha mwanamapinduzi na mzalendo huyu. Nawaombea subira na naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehamu Mosi Tabwe. Amina.”
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269