Breaking News

Your Ad Spot

Apr 4, 2013

NAPE: CHADEMA WANATUMIWA NA AMAFISADI KUMCHAFUA DK. MWAKYEMBE

*Mafisadi wana uchu wa kujipenyeza katikati ya Jitegemee na Mwekezaji kwa faida yao
*Mawasiliano yaliyopo sasa kati ya TPA na Jitegemee ni barua, siyo mkataba
HII NI BARUA SIYO MKATABA: Nape akisema alipozungumza leo
NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ameishukia Chadema na kudai kwamba viongozi Chama hicho wanatumiwa na baadhi ya mafisadi kujaribu kumchafua Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2013, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam, Nape amesema, hatua ya mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema kutoa tuhuma dhidi ya CCM kuwa kupitia kampuni yake ya Jitegemee Trading, imeingia mkataba na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika mradi wa upanuzi wa Bandari Kavu kwa kutumia eneo la SUKITA lililopopia ni uzushi ambao Chadema wamelishwa na mafisadi hao.

Nape alisema tuhuma hizo ambazo zimechapishwa leo Aprili 4, 2013, na baadhi ya vyombo vya habari  hasa Tanzania Daima zikidai Chadema wameibua unaoitwa ufisadi wa Mwakyembe wa kuipa CCM zabuni ya kupanua bandari si za kweli.

Amesema uongo huo Chadema wamelishwa na baadhi ya mafisadi waliotaka kutumia eneo hilo la CCM kujaribu kukaa katikati ya mwekezaji yeyote atakayejitokeza na Jitegemee kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi na kwamba hatua hiyo ni mwendelezo wa Chadema kutumiwa na mafisadi katika kutimiza mambo yao na kutumika huko kunasukumwa na kiu ya Chama hicho kutaka kushika dola kwa gharama yoyote.

Nape alisema kibaya zaidi katika tuhuma hizo, Kiongozi huyo wa Chadema alikwenda mbali kwa kuishutumu Wizara ya Uchukuzi na Waziri wake Dk. Harrison Mwakyembe kwa madai ya kukiuka taratibu na kutoa zabuni ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa CCM tena kinyume na taratibu za manunuzi.

"Ukweli ni kwamba Kampuni ya Jitegemee Trading Company ni mali ya CCM, na pia ni kweli kuwa kiwanja kilichotajwa ni mali ya CCM kilichokombolewa kutoka zilizokuwa mali za SUKITA ambayo pia ilikuwa kampuni ya CCM, lakini TPA na Jitegemee mpaka sasa hawajaingia mkataba wowote.

Alisema ukweli ni  kwamba eneo hilo limeombwa na wawekezaji wengi wakiwemo TPA na masharti waliyopewa wote ni kuwasilisha mapendekezo ya mipango yao ya kibiashara kabla ya kufikiriwa uamuzi wa nani awekeze kwa ubia na Jitegemee kwenye eneo hilo.

"Wanachokiita wenzetu wa Chadema kuwa ati ni zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Jitegemee na Mamlaka ya Bandari ni barua ya TPA kwenda Jitegemee wakiomba ridhaa ya kushirikiana kuliendeleza eneo la kampuni hiyo ya Jitegemee lenye ukubwa wa zaidi ya ekta 100, katika mfumo wa ushirikiano yaani "Joint Venture" kupitia utaratibu wa PPP (Public, Private Partnership) jambo ambalo ni la kawaida sana kwani linafuata utaratibu na sheria zote husika", Nape alifafanua.

Alisema, Chama Cha Mapinduzi kinamiliki Kampuni ya Jitegemee, na kwamba pamoja na umiliki huo, kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli za uwekezaji kwa muda mrefu kwa kufuata taratibu zote na sheria za nchi kwa ujumla.

"Tunatambua kuwa Chadema kwasasa wanapitia wakati mgumu sana kisiasa kutokana na kuanza kuvuna walichopanda kwa muda mrefu katika siasa za nchi yetu. Lakini pia tunatambua tabia ya viongozi wa Chama hicho ya kudandia kila gari linalopita bila kujua linakokwenda kwa kugeuza kila kinachofanyika nchini, ilimradi hakifanywi na wao basi ni haramu", alisema Nape na kuongeza;

"Hata hivyo mazingira hayo wanayopitia Chadema hayawapi uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kutofautisha barua ya maombi ya kushirikiana kuendeleza eneo na mkataba, aidha mazingira wanayopitia kwa sasa hayawapi uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kujua kuwa kinachofanyika ni mawasiliano ya awali sana ya kusudio la kuendeleza eneo husika na hakuna taratibu zilizokiukwa".

Nape alidai umbumbumbu wa aina hiyo unatia mashaka sana juu ya uwezo wa Chadema wa kufikiri na kupambanua mambo na kwamba jambo moja wanaloonekana kulimudu ni uwezo wao wa kutunga uongo na kupanga machafuko. "Na hii ndio siri ya watanzania kuwakataa kila kukicha na ndio siri ya kufa kwa chama hicho, kwani njia ya muongo ni fupi", alisema Nape.

"CCM inachukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Uchukuzi kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya chini ya Dr. Harrison Mwakyembe hasa ya kuongeza ufanisi kwenye bandari yetu ya Dar es salaam. Tunawataka wasikatishwe tamaa na mafisadi wachache, wachape kazi kwa uzalendo huohuo waliouonesha", alisema.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages