Moja ya madarasa katika Shule ya Msingi Dihinda iliyopo
kata ya Mvomero ambalo limejengwa na Shirika la Room to Read.
*Ni shirika pekee lenye mradi wa kuimarisha uwezo wa kusoma,
kuandika na kuhesabu kwa watoto.
*Tayari limefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 60 katika
shule za msingi 15 wilayani Mvomero.
*Sasa laelekeza nguvu zake wilayani Bagamoyo na kukusudia
kujenga madarasa 40 na maktaba 20.
Room to Read ni Shirika la Kimataifa lisilo la kibiashara
linalojishughulisha na kuboresha na kuinua elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa na maktaba pamoja na kusambaza vitabu vya
kujisomea wanafunzi sambamba na kuhamasisha usawa wa kijinsia kwa kuwasaidia wanafunzi wa kike waliopata masomo na kuwainua
kitaaluma katika nchi kadhaa duniani.
Kwa sasa shirika hili limefungua tawi hapa nchini Tanzania
likiwa na program kadhaa za kusaidia kuboresha na kuinua kiwango cha elimu katika shule za msingi.
Mo blog ilipata fursa ya kuzungumza na
Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo nchini Tanzania, ambaye alitoa maelezo ya kina kuanzia historia ya shirika hilo, kuanza kwa shughuli zake
hapa nchini, mafanikio yaliyopatikana na hatimaye mikakati ya shirika hilo katika siku za usoni.
Theodory Mwalongo ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la
Room To Read ambalo ni Shirika la Kimataifa lenye Makao yake makuu huko San Francisco nchini Marekani ambako lilianzishwa mwaka
2000.
Akizungumzia shirika hilo Theodory Mwalongo anasimulia…………………!!
Lilianzia huko nchini Nepal na mwanzilishi wake alikuwa
anaitwa John Wood ambaye alikuwa na Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika la Microsoft na katika shughuli zake aliweza kupita Nepal akaona
mahitaji makubwa ya watoto ya vitabu.
Akaamua kuacha kazi yake ya kutangaza biashara ya
kompyuta huko Asia akaamua kurudi Marekani akawa anakusanya vitabu na kuvipeleka Nepal, lakini alipopeleka vitabu vile ikawa hakuna
mahali pa kuviweka kwa sababu hakukuwa na madarasa hali ilikuwa ni mbaya sana.
Basi akaanzisha wazo la kujenga kwanza madarasa,
kujenga vyumba vya maktaba na baadae kupeleka vitabu.
Basi hatimaye shirika limeena katika nchi nyingi ambapo
kwa sasa Room To Read inafanya kazi zake katika nchi 10 duniani na kwa hapa Afrika ipo katika nchi 3 ambazo ni Afrika Kusini, Zambia na
Tanzania.
Hapa Tanzania shirika limepata usajili wake mwezi wa 9
mwaka 2010 lakini rasmi limeanza shughuli zake mwaka 2011 kwa kazi za kuboresha elimu ya msingi.
Shirika lina programs nne (4); ya kwanza ni kuboresha
miundo mbinu ya shule tukimaanisha ujenzi au ukarabati wa vyumba vya madarasa, kuwawezesha watoto kupata mahali pazuri pa
kujifunzia lakini waalimu pia mahali pazuri pa kufundishia.
Jengo lililokamilika la shule ya msingi Kanga Wilayani
Mvomero tarafa ya Turiani ambalo limejengwa na shirika la Kimataifa la Room to Read.
Sambamba na program hiyo ni uanzishaji wa maktaba
katika shule za msingi. Maktaba hizi zinawekwa vitabu vya hadithi vya watoto na vitabu vya maarifa mengine kama vile mazingira, jinsia,
afya, haki za binadamu na kadhalika.
Kwa hiyo katika uanzishaji wa maktaba tuna program ya
tatu ambayo inalenga uchapaji wa vitabu vya hadithi. Kwa hiyo tunagundua watunzi mahiri na wachoraji wanatunga vitabu vya hadithi za
watoto na kuviweka katika maktaba hizo.
Pia katika program hii ya kuboresha elimu ya msingi, tuna
program ya kushirikiana na walimu katika shule za msingi, waratibu kata na maafisa elimu wa shule za msingi kuimarisha uwezo wa
kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto.
Mwanafunzi akijisomea katika maktaba mpya ya kisasa na
yenye hewa safi iliyojengwa na shirika la Room to Read.
Hivyo hizi program 4 nilizozitaja yaani kuboresha miundo
mbinu katika shule za msingi, uanzishwaji wa maktaba, kuboresha kusoma, kuandika na kuhesabu na kuchapisha vitabu kunalenga katika
shule za msingi tu. Lakini tuna program moja kubwa ambayo inalenga kuwawezesha wasichana waliokosa kwenda elimu ya sekondari
kuendelea na masomo.
Tuna maeneo matatu, kwa kuwasaidia wasichana ambao
wametoka katika familia ambazo zina kipato cha chini kuwalipia ada na mahitaji mengine. Lakini pia kusaidiana na shule husika kuwasaidia
wasichana kuwainua kitaaluma, wale ambao uwezo wao wa kufanya vizuri katika masomo uko chini, basi Room To Read inashirikiana na
waalimu kuweka mikakati ya namna ya kuwainua kufanya vizuri katika masomo.
Na tatu kuna program ya kuwasaidia Stadi za maisha
kuwawezesha wajitambue, waweze kufanya maamuzi sahihi na wajue ni kwa nini wako shuleni. Hivyo basi tungesema tuna program kuu
mbili, kuimarisha elimu ya msingi na program ya wasichana katika sekondari.
Pichani ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read
Tanzania Bw. Theodory Mwalongo akizungumza na baadhi ya wanafunzi wilayani Mvomero wakati wa kukabidhi majengo ya Maktaba za
kujisomea pamoja na madarasa.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania
Bw. Theodory Mwalongo akisoma hotuba yake katika sherehe za kukabidhi majengo ya madarasa na Maktaba katika Wilaya ya Mvomero
tarafa ya Turiani.
Mwalongo anaendelea kutueleza Room to Read kwa
Tanzania limefanya nini…………………?
Sasa katika Tanzania baada ya kupata usajili tulianza katika
katika wilaya ya Mvomero katika tarafa ya Turiani.
Katika kukamilisha hizo program tulizozitaja hapo juu, kwa
mwaka 2012 tuliweza kujenga madarasa 60 katika shule za msingi 15. Katika madarasa hayo 60, vyumba 45 ni vya kusomea darasa la
kwanza, la pili hadi la tatu na vyumba 15 vilijengwa maalum kwa ajili ya kuanzishwa maktaba.
Mradi huu mkubwa ambao uligharimu karibu shilingi bilioni
moja na laki tano (1.5bn) tulishaka kabidhi serikalini, kwa serikali ya wilaya ya Mvomero tarehe 22 mwezi Machi katika sherehe kubwa ya
kufana ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Ndugu Anthony Mtaka ndio alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano
hayo.
Madarasa hayo yameaanza kutumika tayari na maktaba
hizo zinatumika na wananchi wamefurahia sana kitendo hiki. Kwanza tumepunguza msongamano mkubwa sana katika madarasa yale kwa
sababu kabla ya hapo unakuta chumba kimoja cha darasa kina wanafunzi zaidi ya 60 lakini sasa angalao tumepunguza msongamano
huo.
Wanafunzi wa shule ya msingi wilayani Mvomero tarafa ya
Turiani wakiimba na kufurahia baada ya kukabidhiwa rasmi darasa zuri lenye hewa safi pamoja madawati mapya lililojengwa na shirika la
Room to Read.
Lakini kikubwa ni kuwa kwa mara ya kwanza katika historia
ya maeneo yale ni shule kuwa na maktaba, watoto wanafurahia sana kutumia vyumba vile vya kujisomea kwa sababu kuna vitabu vya
hadithi na kadhalika. Walimu nao wamepata unafuu mkubwa wa kuwa na nafasi za kuweza kufundisha. Lakini pia halmashauri ya wilaya
imelipokea vizuri kwamba kwa kweli tumepunguza mzigo mkubwa ambao halmashauri inapambana nao kujenga vyumba vya
madarasa.
Naweza kusema Room To Read ipo hapa Tanzania
kusaidiana na serikali na wadau wengine kuinua ubora wa elimu hapa Tanzania.
Sasa hivi tumeanza katika mkoa wa Pwani ambako tutaanza
na wilaya ya Bagamoyo, ambako mwaka huu tunategemea kuzifikia shule 20 ambapo tunategemea kujenga vyumba vya madarasa 40 na
vyumba vya maktaba 20.
Tutakuwa na program ya kuboresha wasichana na huo
mradi wa kusaidia watoto kujua kusoma na kuandika.
Hii ndio hali halisi ya baadhi ya madarasa katika shule za
wilayani Mvomero tarafa ya Turiani hapo awali.
Mkurugenzi Mwalongo wa Room to Read hakusita kutoa rai kwa
serikali………………..!!!
Rai yangu ni kuiomba serikali kushirikiana na sisi
kuhamasisha wananchi waweze kuchangia fursa ambazo ziko ndani ya uwezo wao, kama vile kuchangia mchanga, mawe, matofali hata
nguvu kazi, lakini pia halmashauri ishirikiane na sisi kuhakikisha majengo yake yanakuwa katika ubora unaotakiwa na shirika liweze kufuata
viwango vya serikali vilivyowekwa.
Naamini kwa mshikamano huo wa serikali, wananchi na sisi
tunaweza tukasaidia kuboresha elimu katika Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269