DODOMA, Tanzania
NAIBU Waziri wa Eliumu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ameonya kuwa serikali itaendelea kuwafukuza vyuoni bila huruma wanafunzi wote watakaokuwa wakibainika kuendesha migomo kwa kuchochewa na wanasiasa.
Waziri Mulugo ametoa kauli hiyo Bungeni lkeo mjini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Jonh Mnyika aliyetaka kujua ni kwanini serikali haijawarudisha wanafunzi wengi waliofukuzwa vyuoni kwa kufanya migomo ikiwemo tatizo la kukosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo.
Mulugo alisema kuna baadhi ya wanasiasa ambao hufika katika baadhi ya vyuo vikuu na kuendesha masuala ya kisiasa kwa mlengo wa uchochezi ikiwa ni pamoja na wanasiasa hao kuwachochea wanafunzi kufanya migomo na maandamano yanayosababisha uvunjifu wa amani na kuharibu mali.
Kwa mujibu wa Mulugo kufanya siasa vyuoni si kosa isipokuwa kushawishi vurugu kwa kuwapandikiza wanafunzi jazba hadi kuzusha vurugu ni kosa ambalo serikali haitaweza kulifumbia macho.
Mulugo aliongeza kuwa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam wanafunzi 99 walibainika kufanya vurugu na kusimamishwa masomo ambapo baada ya uchunguzi 78 walirudishwa huku wengine 21 bado kutokana na uzito wa ushiriki wao.
Aliongeza kuwa katika chuo cha Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Muhimbili wanafunzi 115 walibainika kushiriki vurugu kati yao 81 walipewa onyo kali, 24 walisimamishwa kwa muda wa mwaka mmoja na wanane miaka miwili ambapo watarudi chuoni Desemba mwaka huu na wawili walifukuzwa, wakati Chuo Kikuu cha Dodoma wanafunzi 570 walihusika katika vurugu na hivyo kusimamishwa, kati yao 563 walirudishwa chuoni na saba walifukuzwa moja kwa moja kutokana na uzito wa ushiriki
“Baadhi ya wanasiasa wakiwemo wabunge wamekuwa wakienda vyuoni na kuwachochea wanafunzi sisi tunasema hilo ni kosa, sasa nyinyi kawachocheeni na muwashawishi wagome na wafanye vurugu na sisi tutawafukuza. Sisi ndiyo serikali tunasema hatutasita kumfukuza mwanafunzi yeyote ambaye atabainika kufanya mgomo usio na ulazima kwa kushinikizwa na wanasiasa tutaendelea kuwafukuza wale wote watajkaobainika'' Alisema Mulugo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269