Breaking News

Your Ad Spot

May 1, 2013

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA ALFRED TANDAU

RAIS JAKAYA KIKWETE

Dar es Salaam, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea kushtushwa na kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha aliyekuwa Mweka Hazina wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kiongozi wa miaka mingi wa wafanyakazi na Waziri wa muda mrefu wa Serikali, Mheshimiwa Alfred Tandau ambaye ameaga dunia jioni ya leo, Jumanne, Aprili 30, 2013.

Katika salamu zake kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM amesema:
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mzee Alfred Tandau ambaye nimejulishwa kuwa amepoteza maisha jioni ya leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu ya kansa ya tumbo.”

“Nilimfahamu Mzee Alfred Tandau kwa miaka mingi. Alikuwa kiongozi hodari na mwaminifu ambaye katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wake wa umma alithibitisha uadilifu na uzalendo wa kiwango cha juu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Katika uongozi wa Chama cha Wafanyakazi cha NUTA na baadaye JUWATA, Mzee Tandau alijipembenua kama mtetezi halisi na mkweli wa maslahi ya wafanyakazi. Katika Serikali ambako alitumia kwa miaka mingi kama Waziri alikuwa mwaminifu na mtii kwa Serikali yake, kwa viongozi wake na kwa wananchi aliowatumikia. Katika nafasi yake ya Mweka Hazina wa CCM aliendeleza sifa hizo hizo alizokuwa nazo tokea nyuma. Tutakosa sana busara na ushauri wake.”

Ameelezea Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Kinana salamu zangu za dhati za rambirambi kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako nawatumia rambirambi viongozi na wanachama wote wa CCM kwa kumpoteza kiongozi na mwanachama mwenzao.”

Amesisitiza: “Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie salamu nyingi za pole kwa familia kwa kuondokewa na kiongozi na mhimili wake. Wajulishe kuwa niko nao katika kuomboleza kifo cha kaka yetu na kiongozi mwenzetu na naelewa machungu yao katika kipindi hiki. Napenda wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya marehemu. Amina.”

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages