Breaking News

Your Ad Spot

May 5, 2013

RAIS KIKWETE AWASILI KUWAIT

RAIS KIKWETE

KUWAIT CITY, Kuwait
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Kuwait City mchana wa Jumapili, Mei 5, 2013, kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Taifa la Kuwait kwa mwaliko wa Mfalme wa Kuwait, Amir Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al Sabah.
Ndege ya Rais Kikwete ambaye anaandamana na Mama Salma Kikwete imewasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Amiri, Kuwait City saa saba na nusu za mchana ambako Rais amepokewa na Mfalme – His Highness Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah na viongozi wa juu wa Dola la Kuwait.
Rais amekagua gwaride la heshima la Jeshi la Kuwait kabla ya msafara kuanza safari ya kwenda kwenye Kasri ya Bayan ambako Rais na ujumbe wake umefikia.
Katika ziara hiyo, Rais ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Abdallah Kigoda, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Zanzibar Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais. Fedha, Uchumi na Mipango wa Serikali ya Zanzibar Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee.
Miongoni mwa shughuli kubwa za Rais Kikwete kwenye siku ya leo ya kwanza ya ziara hiyo ya kwanza kufanywa na kiongozi mkuu wa Tanzania katika Kuwait katika historia ni kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na ujumbe wa Taifa la Kuwait ukiongozwa na Mfalme Sheikh Sabah Al Ahmad Al Jaber Al Sabah
Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Kuwait Mheshimiwa Ali Fahad Al Rashed na Waziri Mkuu Mheshimiwa Sheikh Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah. Mazungumzo hayo yatafanyika kwenye Hoteli ya Jahra 3 katika Kasri ya Bayan  ambako Rais na ujumbe wake umefikia.
Baadaye leo usiku, Rais Kikwete atakuwa mgeni rasmi kwenye dhifa ya kitaifa ambayo itaandaliwa kwa heshima yake na Mfalme.
Katika siku ya pili ya ziara yake kesho, Rais Kikwete miongoni mwa mambo mengine atatembelea Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Kuwait katika eneo la Al Ahmadi.
Kuwait ni nchi ya sita duniani kwa kuzalisha mafuta mengi ikiwa inatoa asilimia saba ya mafuta yote duniani na ikiwa na kiasi cha utajiri wa mafuta unaokadiriwa kufikia mapipa bilioni 104 katika eneo lake na lile la bahari kuu ambako inagawanya utajiri huo na nchi jirani ya Saudi Arabia.
Rais Kikwete pia atakutana na kuzungumza na  Bwana Ghanim Sulaiman Al-Ghaniman, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait ambao umegharimia miradi mingi na yenye thamani ya mabilioni ya fedha na hasa ile ya barabara katika Tanzania. Rais pia atakutana na kufanya mazungumzo na Bwana Mohamed Thunyan Al Ghanim, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda katika Kuwait.
Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na Bwana Bader Mohamed Al-Saad wa Mamlaka ya Uwekezaji katika Kuwait na baadaye ataandaliwa chakula cha jioni na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Sheikh Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages