Breaking News

Your Ad Spot

Jun 14, 2013

KINANA AMBURUZA MAHAKAMA KUU MSIGWA

*NI KWA KUMHUSISHA NA UJANGILI, BIASHARA YA PEMBE ZA NDOVU
*ATAKA FIDIA SH. MILIONI 350
PETER MSIGWA
DAR ES SALAAM, Tanzania
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amefungua mashitaka katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) kufuatia mbunge huyo kumhusisha na ujangili na biashara ya pembe za ndovu.

Amefungua kesi hiyo kupitia Wakili wake, Eric Ng'mayo, kutokana na tuhuma alizozitoa Mchungaji Msigwa, dhidi yake kuhusiana na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu.

Katibu mkuu huyo amefungua kesi hiyo kupitia kwa wakili wake Eric Ng'mayo, baada ya mlalamikiwa huyo, kukataa kukanusha na kumuomba radhi dhidi ya tuhuma hizo, hivyo Kinana ameiomba mahakama imwamuru Msigwa kumlipa fidia ya sh. milioni 350.

“Naiomba mahakama imwamuru mlalamikiwa amlipe fidia ya sh. milioni 350 kama hasara rasmi. Pia, fidia ya maudhi na fidia ya hasara, mfano gharama za kesi.

“Mahakama imwamuru mlalamikiwa amlipe riba kwa kiwango cha mahakama kwa tunzo ambayo atapewa na mahakama tangu tarehe ya hukumu hadi malipo ya mwisho na  kufuta tuhuma zake dhidi yangu na aniombe radhi kwa kuchapisha katika magazeti mawili ya Kiingereza na mawili ya Kiswahili yanayosambazwa nchini,” alidai Kinana kupitia hati yake ya madai.

Kupitia hati hiyo ya madai, Kinana anadai mlalamikiwa aliendelea  kurusha tuhuma hizo, hata baada ya kumtaka amuombe radhi.

Mlalamikiwa huyo, ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, anadaiwa kuwa alitoa tuhuma dhidi ya Kinana kwa nyakati tofauti nje na ndani ya Bunge.

Katika hati yake ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo na Wakili Ng'mayo, Kinana anadai kwanza Mchungaji Msigwa, alitoa tuhuma hizo Aprili 21, mwaka huu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Mbugani, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

Pia, inadaiwa mlalamikiwa huyo alirudia shutuma hizo bungeni alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.

Katika hati hiyo, amenukuu maneno yanayodaiwa kutamkwa na Mchungaji Msingwa katika mkutano huo kuwa: "Kinana (naomba waandishi wa habari mnisikie na nyie Usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa kupita barabarani na kuwaambia Watanzania  waiamini CCM. Kinana mikono yake si misafi.

"Hata kwenye NASACO (Shirika la Wakala wa Meli Tanzania) kuna harufu ya ufisadi ndani yake, ajibu hoja... Kinana meli zake ndizo zinazohusika kubeba pembe nchi hii. Hajajibu hoja hizo. Kwa siku nchi hii tembo 67 huuawa." Hao ndio wanaokifadhili Chama Cha Mapinduzi, kina Kinana halafu wanakuja eti kuwashawishi Watanzania muwasikilize na kwamba Chama Cha Mapinduzi eti ni kizuri.

"Halafu leo tukikaa ndani ya Bunge tunapojaribu kuwatetea wananchi tumeacha majimbo yetu. Haya mambo ninayoongea ni hatari kwa sababu haya yote ni majangili ni organized crime. Ni mtandao wa kimataifa, uko duniani kote, unaweza ukatuua, lakini wabunge tumesimama tunawatetea..."

Mlalamikaji huyo anadai kutokana na kauli hizo, ameharibiwa tabia yake na uaminifu na hadhi yake kitaaluma na weledi, hivyo kumfanya achukiwe na kudharauliwa katika jamii.

Aidha, anadai jina lake zuri na heshima yake alivyojijenga katika muda wote wa maisha yake vimeharibiwa na mlalamikiwa kwa nia mbaya.

Kinana anadai tuhuma hizo ni za uongo, licha ya kumsababishia maumivu ya kisaikolojia na hasara kubwa kifedha, kwani kabla ya tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho za mchakato wa mazungumzo ya mradi wa ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji wa kampuni kutoka nje.

Amedai kuwa kutokana na tuhuma hizo, kampuni hiyo ilivunja majadiliano hayo, na kwamba sababu iliyotolewa ya kufanya hivyo ni kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa jangili anayejihusisha na biashara haramu ya pembe za ndovu.

Kinana anadai mradi huo ulikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni nne, hisa zake za ushiriki zilikuwa asilimia 25 katika kipindi cha miaka mitano, hivyo kupata hasara ya sh. milioni 350.

Aidha, mlalamikaji huyo anaiomba mahakama itoe zuio la kudumu kumzuia mlalamikiwa au wakala wake kutoa ua kuchapisha taarifa zozote dhidi yake. 

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages