KIJO BISIMBA |
Mahakama ya Kimataifa ya Kupambana na Uharifu (ICC) imetupilia mbali ombi la kuichunguza Serikali ya Tanzania kwa madai ya kushiriki mauaji ya raia wake na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu na raia.
Mahakama hiyo imetupilia mbali maombi hayo yaliyowasilishwa kwake Septemba mwaka jana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) cha Dar Es Salaam kikiomba Mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi kufungua mchakato wa upelelezi na uchunguzi kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu na makosa ya haki za binadamu yaliyodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama nchini.
Maombi hayo ya LHRC yalikuwa yakiishutumu Serikali kwa kuwa mshiriki na mlinzi wa mauaji hayo yaliyofanywa na vyombo hivyo. Kituo hicho kilidai kuwa angalau kiasi cha watu 237 wameuawa na vyombo hivyo tokea mwaka 2003.
Lakini Jumatano wiki hii, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushahidi katika Ofisi ya Mwendeshaji Mashitaka Mkuu wa ICC, Bwana M.p. Dillon, alikiandikia barua LHRC kukijulisha juu ya uamuzi wa Mahakama hiyo kutokufungua uchunguzi na upelelezi dhidi ya Serikali ya Tanzania kwa sababu hakuna ushahidi wa madai ya kituo hicho.
Kwa mujibu wa Bwana Dillon, masuala yaliyotajwa na LHRC na ushahidi wa dhahiri uliopo haukidhi kiwango cha kuweza kufungua uchunguzi na upelelezi dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Aliongeza kuwa madai dhidi ya Tanzania hayakidhi kiwango wala hayamo ndani ya mamlaka ya Mahakama hiyo kwa sababu hayafikii hatua ya kuweza kuitwa mauaji ya kimbari, wala makosa dhidi ya binadamu ama makosa ya kivita, kama inavyoelezwa katika Vipengele vya 6 hadi 8 vya Katiba ya Rome ya Mahakama hiyo.
Katika barua iliyoandikwa kwa Dkt. Helen Kijo-Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bwana Dillon amesema: “Katika hali hiyo, Mwendeshaji Mashitaka Mkuu, ameamua kuwa hakuna msingi kwa wakati huu wa kuendelea na shughuli hii. Hata hivyo, habari uliyotutumia itabakia kwenye kumbukumbu na nyaraka zetu, na uamuzi wa kutokuendelea na uchunguzi, unaweza kufikiriwa upya endapo utapatikana ukweli zaidi, ushahidi wa nyongeza ama habari mpya.”
Ofisa huyo wa ICC amekishauri LHRC kutafuta haki kupitia vyombo vya haki katika Tanzania ama kuelekeza maombi na madai yake kwenye vyombo husika vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269