Breaking News

Your Ad Spot

Jun 13, 2013

SOMA USHAURI WA JAJI BOMANI KUHUSU MFUMO WA MUUNGANO

JAJI MARK BOMANI
NA BELINDA KWEKA, MAELEZO,DSJ
MWANASHERIA  Mkuu wa Serikali  mstaafu, Jaji Mark Bomani ametoa wito wa kupingwa kwa kura ya maoni kwa wakazi wa Tanzania Visiwani ili kuona kama wanahitaji mfumo gani wa Muungano kabla ya kuendelea na mchakato wa sasa wa rasimu ya Katiba  mpya .

Akizungumza na  waandishi wa  habari leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari –MAELEZO , Jaji Mack   Bomani  alisema  anaipongeza tume ya Jaji  Joseph   Warioba kwa kazi nzuri na pia kwa mapendekezo yake juu ya  Muungano  wa Tanzania.

Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo  Jaji  Bomani  alitoa historia fupi juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo ameeleza kuwa muungano huo ulipendekezwa na hayati Sheikh Abeid  Amani  Karume na hayati Mwalimu  Julius  Nyerere, ambao walikutana mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari, mwaka 1964.

Jaji Bomani   aliongeza  hayati  Karume  alipendelea nchi mbili kuungana  na kuwa  nchi moja , lakini hayati  Nyerere  alisita  kidogo  kwa kuogopa kwamba ingeonekana Zanzibar imemezwa na Tanganyika na pengine kuleta maasi Zanzibar hivyo kupendekeza kuundwa mfumo wa muda mfupi wakati mfumo wa kudumu ukifanyiwa kazi.

 “Suala la Muungano  ndilo  suala kubwa kuliko yote katika  mchakato  wa Katiba mpya.  Niliwahi kuto ushauri nao ni kwamba ifanyike kura ya maoni ya wananchi hasa Zanzibar  kama wanautaka muungano au la na kama wanautaka uwe muungano  wa mfumo gani ? Mpaka sasa maoni ambayo yanasikika ni maoni ya viongozi mara Zanzibar ijitoe kwenye muungano mara tuwe na muungano wa mkataba,” alisema  Jaji Bomani.

Akijibu maswali aliyoulizwa  na waandishi wa habari ,Jaji Mack Bomani amesema katika uundwaji wa Serikali tatu anaamini utaweza kumaliza migogoro inayojitokeza mara kwa mara hasa upande wa Zanzibar kuogopa kumezwa. 

“Woga  wa gharama za mfumo wa Serikali tatu hauna msingi. Inategemea Serikali hizo unazifanya vipi. ipo mifano mingi mno duniani ya miungano ya mfumo mbalimbali,” alisisitiza.

Pia ameongezea kuwa kama kutaundwa Serikali tatu basi iwe Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. 

Akiongezea kuhusu katiba mpya amesema “kwa maoni yangu si lazima kazi hii ya katiba iishe kabla ya 2015, tupate muda wa kutosha ili tuweze kupata katiba ya kueleweka na kukubalika na kila mtu”

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages