Breaking News

Your Ad Spot

Jul 11, 2013

LOWASSA AHUTUBIA MKUTANO UMOJA WA MATAIFA, AWASEMEA WAZEE

 Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa akizungumza wakati wa majadiliano yaliyohusu namna ya kuingiza  suala la wazee katika ajenda mpya za Maendeleo baada ya mwaka 2015. Mkutano huo ulioambatana na chakula cha mchana ulifanyika  siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya  Umoja wa Mataifa na ulioandaliwa na United Nations Foundation kwa kushirikiana na  Mashirika mengine ya Kimataifa.  katika mchango wake, Mhe. Lowassa amesisitiza umuhimu wa  ubia kati ya serikali na  sekta binafsi katika kuzikabili changamoto za ongezeko la idadi ya  wazee  duniani. Inasemekana miaka michache ijayo  idadi ya wazee duniani itazidi idadi ya watoto wadogo chini ya miaka mitano.  Pamoja na Mhe. Lowassa wengine waliochangia majadiliano hayo ni  Bi. Ann Pawliczko kutoka UNFPA wa pili kutoka  kushoto, Bw. Jack T. Watters kutoka Pfizer, Bw. Paul Ong HelpAge International, Bw. Sharig Khoja kutoka United Nations Foundation, aliyeketi karibu na Mhe. Lowassa ni Bi. Jane Barratt aliyeratibu majadiliano hayo.

Na Mwandishi Maalum, NEW YORK
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ( Mb) amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo kwa  ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto zinazotokana na ongezeko  kubwa la idadi ya wazee.

“ Maisha Zaidi ya miaka 60   hayapashwi kuwa ya utegemezi, unyonge,  kutojiweza au  kutokuwa na  matumaini.   Wazee bado na wanao mchango  mkubwa  ndani ya  jumuiya,  jamii,   na  familia zao ili mradi tu wawezeshwe”.

Na kwa sababu hiyo anasema Mhe, Lowassa, juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali   katika  nchi zilizoendelea na zinazoendelea  Tanzania ikiwamo za utoaji wa huduma za msingi kama vile  Afya , pensheni na uwezeshwaji zinapashwa kuchagizwa na sekta binafsi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, na  Waziri Mkuu  Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa (Mb ), ameyasema hayo siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati aliposhiriki  majadiliano  kuhusu namna gani suala la  Wazee linavyoweza kuingizwa katika ajenda za maendeleo baada ya mwaka 2015.

Majadiliano hayo  yaliandaliwa na   United Nations Foundation kwa ubia na International Federation of Ageing,   Help Age International,  AARP, Global Coalition on Aging, mHealth Alliance na Pfizer

“Kama  kundi hili la  wazee likiwezeshwa na kusaidiwa ipasavyo , linaweza kuipatia jamii soko jipya,  ujasiriamali,  utoaji wa maamuzi, utoaji wa huduma na  utalaamu  anuai katika maeneo ya sayansi, teknolojia na  upatanishi” anasema  Lowassa.

Na kuongeza, ili hayo yote na mengine mengi yaweze kufanikiwa panahitajika  bajeti ya kutosha  kwa ajili ya kundi hilo la jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya  pensheni, huduma za afya ambazo zitakidhi mahitaji ya wazee, huduma za kisaikolojia na huduma za ulinzi jamii,.
Hata hivyo anasema, inasikitisha kwamba, katika nchi nyingi za Afrika na nyinginezo hata zile zilizoendelea bado  haziwezi kutoa huduma za uhakika na zenye viwango vya kukidhi mahitajio ya wazee.

“Mara nyingi huduma kwaajili ya wazee inabidi zishindane na huduma za makundi mengine kama vile  ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira,  upunguzaji wa  vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito. Hata hivyo pamoja na changamoto zote hizi za vipaumbele hatuwezi kuendelea na utaratibu  huu wa kuchagua. Lazima tutumie maandalizi ya  ajenda za maendeleo baada ya 2015 kuwahudumia wazee” anasisitiza Lowassa.

Akasema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kujikumbusha na kujifunza kwa kosa la kutoingiza suala la Wazee katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayoelekea ukingoni,  kwa  kuhakikisha kwamba Wazee wanaingizwa katika   malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015 kwa kuwa ni suala ambalo haliepukiki.

Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwahudumia wazee, Mhe. Lowassa anasema kama ilivyo kwa  nchi nyingine, Tanzania nayo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee.

Kwa mfano, amesema asilimia 4.5 ya idadi ya watu, ni watu walio na  umri wa miaka 65  wastani  wa juu zaidi  kuliko ule wa asilimia 3.6  Afrika  Kusini mwa Jangwa la  Sahara.

“ Asilimia 80 ya  watu hawa wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo. Serikali  inajitahidi kadri iwezavyo kutoa huduma za msingi kwa kundi hilo  ingawa pia, na kama ilivyo kwa nchi nyingine, tunakabiliwa na changamoto nyingi kukidhi mahitaji yote ya wazee”. Akabainisha.

Akatumia pia fursa hiyo kuyashukuru mashirika ya kimataifa kama vile Help Age International ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake nchi nchi  tangu mwaka 1993.

Akatoa mfano kwa kusema  Shirika hilo,  mwezi  Juni mwaka huu kwa kushirikia na Pfizer limezindua mpango wa miaka miwili  wa kupunguza athari zitokanazo na  magonjwa yasiyoambukiza (NCD) ambayo yamekuwa yakiwaathiri wazee.

Akasema  utoaji wa huduma hiyo unakwenda sambamba na    juhudi za serikali katika kukabiliana na  magonjwa hayo.

Akatoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo na kwamba serikali itakuwa tayari kushirikiano nayo.

Takwimu kutoka  Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ( UNFPA) zinaonyesha kwamba,  katika kila sekunde watu wawili duniani wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwao, na kwa mwaka   karibu watu milioni 58 wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa.

Aidha katika kila watu nane,  mmoja ana miaka 60 au zaidi na makadirio yanaonyesha kwamba ifikapo mwaka  2050 katika kila watu  watano mmoja atakuwa na miaka 60 au zaidi.

Ongezeko la  idadi ya wazee duniani linachangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na  ongezeko la umri wa kuishi ambapo katika nchi 33  raia wao wanaishi zaidi ya miaka 80 wakati miaka mitano iliyopita nchi ambazo  umri wa kuishi  ulifika miaka 80 zilikuwa 19 tu.

Utafiti zaidi unaonyesha , umri wa kuishi  utaongezea  hadi kufikia miaka 90 au hata miaka 100. Japani  kwa sasa ndiyo inasemekana  kuongoza kwa  kuwa na asilimia 30 ya wazee lakini ifikipo mwaka 2050  nchi 64 zitaungana na Japani kwa kuwa na  asilimia 30 au zaidi ya wazee.

 PICHA ZAIDI
Mhe. Lowassa akipeana  mkono na mmoja wa waandaji wa majadiliano hayo kuhusu Wazee, takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la  Idadi ya Watu ( UNFPA) zinazonyesha kwamba mwaka 1950  idadi ya wazee  duniani waliokuwa na  miaka 60 au kuzidi ilikuwa milioni 205, 2012 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 810 milioni. Inakadiriwa kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia  Bilioni 1 si zaidi ya miaka  kumi ijayo na ifikapo mwaka 2050  idadi ya wazee  wenye umri wa miaka 60 na kuendelea itafikia bilioni 2.  Aidha duniani kote wanawake ndio wanaokadiriwa kuishi umri mrefu zaidi kuliko wanaume.
  Mhe. Edward Lowassa akibadilishana mawazo na Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa, Bw. Chitsaka  Chipaziwa
 Mhe. Lowassa akiwa na Balozi wa Pakistani katika Umoja wa Mataifa Bw. Masood Khan
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Edward Lowassa akisalimiana na Balozi wa  Ugiriki katika Umoja wa Mataifa, Bw. Michael Spinellis 
 Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo
Mh. Lowasa kiwa na mmoja wa washiriki wa  majadiliano  kuhusu mstakabali wa wazee

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages