Na Chibura Makorongo, Simiyu
Zaidi ya hekari tisa za mazao ya dengu katika kijiji cha Mwamagulu wilayani Busega mkoani Simiyu zimeteketezwa kwa kufyekwa na maofisa maliasili na misitu kutoka wilaya ya jirani ya magu kwa madai ya kuwa mashamba hayo yapo kwenye hifadhi ya msitu wa Sayaka wilayani humo.
Wananchi wa kijiji hicho walisema ilikuwa tarehe 22 Julai mwaka huu mafiasa misitu wakiongozwa na afisa anayejulikana kwa jina la Mawalwa wakiwa na maaskari na vijana wapatao 30 walivamia mashamba hayo na kuanza kukatakata mazao huku maaskari polisi wakiwa wamesheheni silaha na mabomu ya machozi.
Diwani wa kata ya Nyaluhande Maridadi Sabuni alisema kuwa kumekuwepo na mgogoro mkubwa kati ya wananchi hao na hifadhi hiyo na wanakijiji hao wanadai mpaka wa hifadhi hiyo uko mbali na hujafikiwa na mashamba yao lakini cha kushangaza waliona magari yakivamia mashamba hayo na kuanza kuyateketeza kwa kukata mazao.
Alisema zaidi ya hekari tisa zenye jumla ya kiasi cha milioni sita zimekatwa na wananchi hao wanategemea mazao hayo kwa ajili yta kuweza kupata mahitaji yao ikiwa na pamoja na kusomeshea watoto shuleni na kuynuza ili kuweza kununulia vyakula.
Mbunge wa jimbo la Busenga Dr.Titus Kamani alisema kuwa tatizo hilo linatokana na chuki binafsi na kwamba wilaya ya magu walivamia bila kuonana na uongozi husika kwani eneo hilo lipo katika mkoa wa simiyu wala sio mkoa wa mwanza ambapo alisema kuwa huo ni uvamizi wa kiutendaji wa kazi kwani wilaya ya Busega ni wilaya halali na inawatendaji wake.
Alisema kuwa ataongea na mkuu wa wilaya ya Magu ili kuweza kuwapatia maelezo kamili juu ya uvamizi huo ili kuweza kuona ni jinsi gani ya kuweza kuwasaidia wahanga wa tukio hilo na alimuomba mkuu wa wilaya ya busega kumwandikia barua mkuu wa wilaya ya magu ili kuweza kulitatua tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269