Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Kanda ya Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson, ameanza ziara maalum katika DRC na Kanda ya Maziwa Makuu akiongoza ujumbe mzito unaolenga kutafuta suluhu ya kidiplomasi baada ya kurejea upya kwa mapigano makali katika eneo la Mashariki mw DRC hali ambayo imelifanya eneo la Maziwa Makuu kuwa katika wasiwasi. Mapigano ya wiki iliyopita yalikuwa baina ya Kundi la waasi la M23 na FARD ambayo ni Majeshi ya DRC yakisaidiwa na Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO) Ujumbe wa Bi. Robinson unawahusisha wawakilishi kutoka AU, EU, USA na UN
-----------------
Na Mwandishi Maalum,New York
Kufuatia kurejea tena kwa mapigano makali yaliyotokea wiki iliyopita kati ya majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( FARD) yakisaidiwa na Jeshi la MONUSCO na kundi la waasi la M23. Umoja wa Mataifa sasa unajaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia inayolenga katika kujaribu kuweka sawa hali ya mambo.
Mapingano hayo ambayo siyo tu yanasadikiwa kuliondoa kundi la M23 katika ngome yake ya vilima vya Kibati Magharibi ya Kivu. Yamelaaniwa vikali na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu Ban ki Moon hasa baada ya kundi hilo la M23 kusababisha kifo cha mwanajeshi Mtanzania na kujeruhi wengine kumi wakiwamo wanajeshi kutoka Afrika ya Kusini.
Mchakato huo wa kisiasa unafanywa na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Kanda ya Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson, ambaye amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya jumapili na kutoa rambirambi zake kwa wahanga wa mapigano hayo.
Taarifa kutoka ofisi ya Mjumbe huyo Maalum, inataarifu kwamba, Katika mchakato huo wa kutafuta suluhu ya kidiplomasia , Mary Robinson ataongoza ujumbe maalum utakaowahusisha Mwakilishi wa Umoja wa Afrika, Bw. Boubacar Diaraa, Bw. Russ Feigold, ambaye ni Mjumbe Maalum wa Serikali ya Marekani katika Eneo la Maziwa Makuu, Bw. Martin Kobler Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu katika DRC na Mkuu wa MONUSCO, wakati Jumuiya ya Ulaya itawakilishwa na Mratibu Mwandamizi katika Maziwa Makuu, Bw. Koen Vervaeke.
Kabla ya kuungana na ujumbe huo, Bi. Mary Robison atafanya mazungumzo ya ndani na washirika wa Umoja wa Mataifa katika DRC na kisha atakwenda Goma kama hatua ya kuonyesha mshikamano wake na wananchi wa eneo hilo na Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa ( MONUSCO).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Bi Mary Robison ziara ya Mjumbe huyo na ujumbe wake, pamoja na kutembelea DRC pia watakwenda Uganda na Rwanda kati ya Septemba 4-7, ambapo pamoja na mambo mengine watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa, wawakilishi wa Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Kiraia pamoja na kuhudhuriwa kikao cha dharura cha Mkutano wa Kimataifa wa Kanda ya Maziwa Makuu ( IGCLR).
Taarifa hiyo inabainisha kwamba akiwa katika nchi hizo, Bi. Mary Robinson atasisitiza haja na umuhimu wa pande zinazohusika kusitisha vitendo vya uhasama na kuelekeza nguvu zao katika majadiliano ya kisasa pamoja na mchakato wa Kampala ( Kampala Process).
Aidha inaelezwa kwamba wakati Bi. Robison na ujumbe wake watakapohudhuria mkutano wa IGCLR utakaofanyika Septemba 5 jijini Kampala, watahimiza uharaka wa utekelezaji wa Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, usalama na maendeleo katika DRC na Eneo la Maziwa Makuu, mpango ambao ulisainiwa mapema mwaka huu na nchi 11 na wadhamini wanne wa kimataifa .
Ziara hiyo ya Bi. Mary Robison na ujumbe wake inafuatia kurejea upya kwa mapigano makali katika eneo la Mashariki ya DRC mapigano ambayo yameifanya hali ya mambo katika eneo la Maziwa Mkuu kuwa tete, huku kukiwa na ongezeko kubwa la wakimbizi, hali inayochagiza uharaka wa kutafuta suluhu ya kisiasa ili kurejesha hali ya utengamano katika DRC na eneo la Maziwa Makuu.
Your Ad Spot
Sep 3, 2013
Home
Unlabelled
BAADA YA MAPIGANO MAKALI MASHARIKI MWA DRC UMOJA WA MATAIFA WATAFUTA SULUHU YA KIDIPLOMASIA
BAADA YA MAPIGANO MAKALI MASHARIKI MWA DRC UMOJA WA MATAIFA WATAFUTA SULUHU YA KIDIPLOMASIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269