Breaking News

Your Ad Spot

Oct 27, 2013

BALAA CHADEMA

NA LILIAN JOEL, ARUSHA
BARAZA la uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini kimemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba (pichani) kwa tuhuma za kukihujumu chama hicho

Uamuzi huo ulitangazwa jana mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse aliyesema Mwigamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la ushauri mkoa wa Arusha amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi dhidi yake.

“Iwapo tuhuma dhidi yake zitathibitishwa, hatua zingine za kinidhamu zitachukuliwa kwa kufuata taratibu, kanuni na katiba ya chama,” alisema Natse ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Karatu

Alisema kiongozi huyo amesimamishwa kwa kukiuka sura kumi, kifungu cha 10.1, kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi.

Akizungumza mbele ya baadhi ya wajumbe wa baraza la uongozi Kanda ya Kaskazini wakiwemi wabunge, Grace Kiwelu, Joyce Mukhya, Rebeca Mngodo na Cecilia Paresso, Natse alisema sura na vifungu hivyo vinazuia viongozi wa chama hicho kutuhumiana nje ya vikao halali vya kikanuni na kikatiba.

Pamoja na mambo mengine, Mwigamba anadaiwa kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii Forum ambapo aliwatuhumu viongozi wa kitaifa wa chama hicho kuchakachua katiba katika kipengele cha ukomo wa uongozi.

Katika andiko lake kwenye JF, Mwigamba anatuhumiwa kusema Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willroad Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.

Ingawa haikuweza kuthibitishwa, inadaiwa baada ya Mwigamba aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kikao cha baraza la uongozi Kanda ya Kaskazini waliokuwa wakikutana jijini Arusha kuanzia juzi kubainika kurusha taarifa kwenye mitandao wakati kikao kikiendelea, kulitokea tafrani ya kurushiana maneno na ngumi.

Katika tafrani hiyo, Mwigamba anadaiwa kumtolea maneno ya kashfa na matusi pamoja na kumrushia ngumi mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kabla ya kudhibitiwa na walinzi wa chama hicho maarufu kama Red Bridged.

Lema alithibitisha kutukanwa na kurushiwa ngumi na Mwigamba ingawa alidai haikumpata kwa sababu aliikwepa.

“Ni kweli alinirushia ngumi lakini niliikwepa kutokana na kumuona lengo lake tangu alipokuwa akinikaribia baada ya mimi kumtaka asalimishe kompyuta yake mpakato (Lap top) ili vijana wetu wa IT walikague,” alisema Lema

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alithibitisha Mwigamba kukaidi agizo la kumtaka akabidhi Lap top yake kwa ukaguzi hadi alipodhibitiwa na Red Bredged ambapo baada ya uchunguzi ilibainika kuwa alikuwa akituma taarifa za uongozi na uchanganishi dhidi ya viongozi wakati kikao kikiendelea.

“Baada ya kujiridhisha na ushahidi kuwa ndiye aliyetuma taarifa hizo kwenye mtandao, tuliita polisi na kumkabidhi kwa ajili uchunguzi zaidi na usalama wake,” alisema Golugwa ambaye ndiye mlalamikaji katika shauri lililofunguliwa polisi.

Mwigamba amekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha kuanzia mwaka 2009 amekuwa akishiriki harakati nyingi za chama hicho ambapo hivi sasa anakabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi mahamakani.

Juhudi za kumtafuta Mwigamba kwa ajili ya kuzungumzia taarifa hizo jana ziligonga mwamba kutokana na simu yake ya kiganjani kuzimwa kutwa nzima ya jana.

Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatika jana zinaeleza kuwa Mwigamba aliachiwa kwa dhamana baada ya kusota rumande kwa saa kadhaa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages