ARUSHA, Tanzania
SAKATA la kupigwa na kusimamishwa kwa uanachama kwa mwenyekiti wa Chadema Arusha Samson Mwigamba kwa tuhuma za usaliti wa chama limeendelea kuzua kizazaa baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Arusha Dominick Mboya kusema chama hicho kimejaa udikteta na kutaja orodha ya viongozi na wanachama waliowahi kufanyiwa umafya.
Mboya ambaye awali alikua mwenyekiti wa chama hicho kata ya Elerai amese leo kwamba tukio hilo lililomkuta Mwigamba liliwahi kumkumba hata yeye pale alipokua akiungana na Mwigamba katika kudai utekelezaji wa katiba ya chama kwa kudai kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi mkoa wa Arusha.
Alisema wakati huo Mwigamba alikua ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa yeye akiwa mwenyekiti wa kata hali iliyosababisha viongozi wakuu wa chama hicho kujaribu kuwanyamazisha hadi kufikia kupewa rushwa ya cheo cha uenyekiti wa wilaya bila kufanyika kwa uchaguzi.
Alisema siku chache kabla ya kuelezwa kuhusu uteuzi wake wa uenyekiti ambao ulikua kinyume na katiba alipigiwa simu na kiongozi mmoja akitaarifiwa kupewa nafasi hiyo na kutakiwa kuhudhuria mkutano uliofanyika katika hoteli ya Stereo ili atangaziwe rasmi yeye na wanachama wengine.
Alisema mara baada ya kufika katika mkutano huo alitamkiwa kuhusu uteuzi wake hali ambayo pia hakuifurahia kwakuona kama amekuwa msaliti wa wanachama na viongozi wenzake waliokuwa wakipambania kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi kama katiba inavyotaka.
Alisema baada kuona hilo alikata waziwazi uteuzi huo kwakua umekiuka katiba kwakua hakuna mwenyekiti wa kuteuliwa bali wa kuchaguliwa na pia atakua msaliti kwa kukubali rushwa ya cheo ili kufumbia macho ukiukwaji wa katiba.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho viongozi wote wa kuteuliwa wanakaa madarakani kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja kisha uchaguzi kufanyika lakini kwasasa anashangaa kuona viongozi wa kuteuliwa wanakaa madarakani milele.
Aliongeza kuwa mara baada ya kukataa cheo hicho alitolewa katika ukumbi huo kwa vurugu chini ya ulinzi wa vijana wa ulinzi wa Red Briged ambapo pia walimpora mali zake mbalimbali zikiwemo simu mbili pamoja na fedha taslimu.
Alisema tukio la Mwigamba siyo la kwanza na wala halitakua la mwisho kwakua wapo wanachama na viongozi wengi tu waliofukuzwa,kutekwa na kuporwa pindi wanaposema ukweli au kukosoa uongozi wa juu wa chama hicho.
Aliwataja viongozi waliofanyiwa umafya kuwa ni Bakari Kasembe aliyekuwa katibu wa chama hicho wilaya ya Arusha na katibu mwingine aliyefuatia aliyemtaja kwa jina moja la Credo pamoja na Gerald Majengo aliyekua mwenyekiti wa chama hicho kata ya Terati.
Pia aliwataja vijana wawili wa Red Briged waliokihama chama hicho na kujiunga na CCM baada ya kutekwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ambao ni Nicholaus Kiyeuyeu baada ya vijana hao kutofautiana kimawazo na viongozi wa chama hicho ngazi mbalimbali.
“huku Chadema bwana ukiwa msema ukweli na muwazi katika baadhi ya mambo yanayowahusu viongozi utapigwa tuu siyo kama vyama vingine vilivyokomaa kama CCM hakuna mambo haya wala hakuna udikteta”alisema Mboya.
Alisema kutokana na vitendo hivyo viongozi na wanachama wengi akiwemo yeye wameamua kujiweka pembeni ili kujionea vitendo viovu vinavyofanyika ambapo aliahidi kumpokea Mwigamba katika kambi yao ya waliojiengua kutoka Chadema.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269