Mradi wa ukarabati wa uwanja wa michezo wa namfua uliopo Singida mjini umechelewa kuanza kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kitendo cha Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida kuchelewa kutoa baraka zake juu ya ukarabati huo.
Kwa mujibu wa barua ya kukumbushia iliyotoka kampuni ya Mohammed Enterprises (T) ltd ya Julai 10 mwaka huu kwenda kwa katibu CCM Mkoa,kampuni ya Mohammed Enterprises kwa ushirikiano na Airtel Tanzania,ilikiomba Chama Cha Mapinduzi kiwe sehemu ya makubaliano kwa mkataba wa awali.
Meneja wa kampuni ya Mohammed Enterprises tawi la Mkoa wa Singida, Hassan Mazala amesema barua hiyo ya marudio,ilipokelewa na ofisi ya katibu CCM mkoa wa Singida Julai 15 mwaka huu.Barua ya awali ilitumwa kwa katibu huyo,mapema mwaka huu. Akifafanua zaidi,Mazala amesema kwa vile uwanja wa namfua ni mali ya Chama Cha Mapinduzi,walikiomba kiridhie au kiwe sehemu ya makubaliano kwa mkataba wa awali.
Amesema kampuni ya Mohammed Enterprises imekubali kutoa msaada wa shilingi 620 milioni na Airtel Tanzania,itatoa shilingi 820 milioni kugharamia ukarabati huo. "Ukarabati huo unatarajiwa kuwa ni ujenzi wa kuta za uwanja kwa ndani na majukwaa ya kukaa watazamaji,uwanja wa kuchezea mpira wa miguu,eneo la kukimbilia riadha.Pia ukarabati wa vyoo jukwa kuu na maeneo mengine kadri itakavyoonekana inafaa"alifafanua Mazala ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu (NEC) CCM taifa manispaa ya Singida.
Amesema makampuni hayo mawili yanajitolea kukarabari uwanja wa namfua kwa gharama ya zaidi ya shilingi 1.4 bilioni,machi mwaka huu,makampuni hayo yalituma wataalam kuja kufanya upembeuzi yakinifu,lakini wataalam hao warudi waliko toka,kwa sababu CCM hadi sasa bado haijaridhia shughuli za ukarabati wa uwanja wake.
Mazala amesema hofu yake ni kwamba ucheleweshaji huo,kwanza athari zake ni kwamba gharama inaweza kuongezeka kutokana na tabia ya dola ya kimerekani kupanda na kushuka.Pia wafadhili hao wanaweza kukwazwa na kitendo cha urasimu.
Katika hatua nyingine,oktoba mosi mwaka huu,mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida,Mgana Msindai,akiwa anazungumza kwenye kilele cha siku ya wazee duniani,aliwataka wananchi kupuuza maneno yanayoenezwa kwamba kampuni ya Mohammed Enterprises na Airtel Tanzania,watakarabati uwanja wa namfua.
Alidai kuwa watu wanaoeneza maneno hayo,ni waongo wakubwa. Hata hivyo, mwenyekiti huyo kabla sherehe za wazee hazijaisha,alibadili kauli yake hiyo na kudai kwamba ameongea kwa simu na CCM makao makuu,wameridhia makampuni hayo yakarabati uwanja wa Namfua.
Uwanja wa michezo wa Namfua unaomilikiwa na CCM mkoa wa Singida, unatotarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa na makampuni ya Mohammed Entreprises (T) ltd ikishirikiana na Airtel Tanzania.Ukarabati huo unatarajiwa kugharimu makampuni hayo zaidi ya shilingi 1.4 bilioni.(Picha na Nathaniel Limu).
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269