Breaking News

Your Ad Spot

Nov 10, 2013

JK AMPA RUNGU MAGUFULI

Amtaka kusimamia sheria barabara zinazojngwa zidumu
GEITA,Tanzania
Rais Dk. Jakaya Kikwete amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama Barabarani inasimamiwa vizuri kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa nchini zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Rais Kikwete akiwa na Mgufuli kwenye hafla hiyo

Akizungumza katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati akizindua ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi Biharamulo yenye urefu wa kilometa 67, Rais Kikwete alisema kuwa wizara ya Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia sheria zilizopo na hasa hii ya kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango vilivyoainishwa katika Sheria Namba 30 ya Mwaka 1973.

Akisistiza umuhimu wa kutunza barabara Rais Kikwete alibainisha kuwa “adui wakuu watatu wanao sababisha barabara kuharibika mapema ni; magari yanayobeba mizigo zaidi ya uzito uliowekwa kisheria, ujenzi duni usiozingatia viwango na kuachwa kwa maji kuzagaa barabarani”.

Wakati huo huo Rais Kikwete alielezea kufurahishwa kwa kuanza ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi ya watu waliokuwa waliokuwa wakieneza taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.

Awali akitoa maelezo ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale alielezea kuwa mradi mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegharimu Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

“Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27 na hivyo kukamilika mwezi Februari mwaka 2015” alisema Injinia Mfugale.

Naye Magufuli alimhakikishia Rais Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha kuwa inamsimamia mjenzi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili aukamilishe kwa muda na viwango vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya nyongeza ya gharama.

Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi yake, Waziri Magufuli alibainisha kuwa wananchi wa mikoa  ya Geita na Kagera wamefurahishwa sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina lami kwa barabara inayounganisha mikoa hiyo ya ziwa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages