KHAMIS MGEJA |
KAHAMA, Tanzania
MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation
nchini, Khamis Mgeja amepinga kauli iliyotolewa na waziri mkuu mstaafu,
Fredrick Sumaye akidai kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete katika vita dhidi ya
rushwa nchini na kwa lengo la kuonesha ni miongoni mwa watu wanaochukizwa na
vitendo hivyo.
FREDERICK SUMAYE |
Akizungumza na waandishi wa habari leo
kijijini kwake Nyanhembe kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Mgeja ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, leo
alielezea kushangazwa kwake na kauli hiyo na kueleza siyo kweli Sumaye
anaichukia rushwa kama alivyodai kwa vile wakati akiwa waziri mkuu ariruhusu kufanyika
mambo mengi yaliyokuwa yakiashiria mianya ya rushwa.
Alisema katika kipindi hicho, Tanzania ndipo
ilipofunga mikataba mingi mibovu katika sekta ya madini, viwanda, mashamba na
ranchi za taifa ikiwemo uuzwaji wa benki ya umma (NBC) iliyouzwa kwa bei ya
kutupa ikiwa ni mikataba iliyofungwa kutokana na rushwa kubwa.
“Binafsi napingana na Sumaye katika hili, siyo
kweli anachukizwa na tatizo la rushwa hapa nchini kama kweli angekuwa na sifa
hiyo basi wakati wa kipindi cha uongozi wake asingeruhusu nchi yetu kufunga
mikataba mibovu, leo hii watanzania wanalia kwa mikataba mibovu iliyofungwa
wakati wake,”
“Katika kipindi chake rushwa ilikuwa kubwa
sana, hata rushwa ya ngono ilishamiri wakati huo ili mtu aweze kupata ajira,
kama anabisha mimi nitamtajia watu waliopewa ajira wake wake baada ya kutoa
rushwa ya ngono, leo hii usafi anaodai anao uko wapi,”
“Mimi nampa ushauri wa bure ni vizuri aache
kupaparika akae chini atulie, maana kauli zake anazozitoa hivi sasa anaonekana
amekuwa ni mtu wa kulalamika kila siku, hatoi ushauri nini kifanyike ili
tufikie mafanikio, asiwakumbushe watu vidonda alivyowasababishia wakati wa
uongozi wake,” alieleza Mgeja.
Mgeja alielezea kushangazwa kwake ni kitendo
cha vyombo vya dola kuendelea kufukuzana na vidagaa huku vikiwaacha mapapa
waliosababisha nchi kuingia katika matatizo makubwa ikiwemo wizi wa fedha za
EPA, Meremeta, mikataba ya Songas na IPTL ambayo yote yalifanyika wakati wa
Sumaye.
“Tunashangaa hii nguvu ya kuwasonta vidole
wenzake anaipata wapi au ana lengo la kufunika madhambi yake aliyoyafanya
wakati akiwa waziri mkuu, lakini suala la rushwa analopigia kelele hakuna
mtanzania anayelipinga wote tunakerwa na rushwa, ni vizuri angeonesha mfano
mzuri kwa kukemea mikataba mibovu iliyofungwa katika kipindi chake,” alisema
Mgeja.
Alisema uingiaji wa mikataba mibovu inayoiumiza
nchi hivi sasa ni rushwa kubwa kushinda rushwa ndogondogo anazozipigia kelele
Sumaye na kwamba huenda kinachosababisha apige kelele na kutapatapa ni baada ya
kuangushwa kwenye uchaguzi wa mjumbe wa NEC wilayani Hanang mkoani Manyara
ambako alishindwa na Mary Nagu.
Pia Mgeja alitoa mfano wa maamuzi mabovu
yaliyofanyika kipindi cha uongozi wa Sumaye kwa kuamua kuuza nyumba za umma
zilizojengwa kwa nguvu ya watanzania wote wakiwemo wafugaji, wavuvi na wakulima
ambao hawakushirikishwa katika kufikia maamuzi ya kuuzwa kwake na badala yake
waliokumbuka ni wafanyakazi peke yao.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari
iwapo hivi sasa yupo katika harakati za kumfanyia kampeni mmoja wa watu
wanaotaka kuwania urais nchini, Mgeja alisema yeye binafsi haamini kama ni
wakati muafaka wa watanzania kuanza kulumbana juu ya mtu gani awe Rais mwaka
2015.
“Mimi nafikiri suala nani awe rais mwaka 2015
siyo wakati wakati hivi sasa, na halipaswi kupewa nafasi ya kusababisha
watanzania tugawanyike, tujengeane uhasama, chuki na fitina na kusababisha
kupoteza umoja na mshikamano wetu tulionao, maana urais unapangwa na mungu
mwenyewe yeye ndiye anayemjua rais ajaye atakuwa nani,” alisema Mgeja.
Alisema suala la rais ajaye tayari limo ndani
ya mioyo ya watanzania, ndiyo wanaojua ni nani atakuwa rais wao baada ya Rais
Kikwete, hakuna sababu ya kulumbana na
kwamba iwapo kelele za Sumaye ni juu ya kutaka kuwania urais mwaka 2015, ni
vizuri akawaachia wananchi wenyewe ndiyo wataamua wakati utakapofika.
“Kama kelele hizi za mwenzetu ni urais wa mwaka
2015, tunamshauri aache kupapalika, akae chini atulie, na asiwasonte vidole
vibaya wenzake, hakuna mtantania mwenye hatimiliki ya urais hapa nchini, wote
wana haki sawa, ni juu ya watanzania wenyewe kuamua rais wao awe nani,” alisema
Mgeja.
Hata hivyo mwenyekiti huyo ambaye taasisi yake
inashughulika na masuala ya utawala bora, utamaduni, michezo na haki za
binadamu alisema ni vizuri rais ajaye awe na sifa mbili kuu moja ni kuwekeza
hisa za imani kwa watanzania, anayeaminika na sifa ya ziada iwe ni uwezo wa
kutatua changamoto zilizopo nchini.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269