Breaking News

Your Ad Spot

Dec 27, 2013

KIJANA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUDAIWA KUZITANDIKA POMBE KRISMAS

Chibula Makorongo, Shy, Tanzania
Kijana  aliyejulikana  kwa jina la Godi Shaini Fanuel Mangala (34) mkazi  wa mtaa wa Majengo Mapya  kata ya Ngokolo mjini Shinyanga amefariki dunia huku ikidaiwa kuwa chanzo ni kunywa viroba vingi kupita kiasi.
 
Tukio hilo limetokea Desemba 25 mwaka huu siku ya Krismasi  majira ya saa moja jioni ambapo marehemu ambaye pia ni mfanyakazi wa kampuni ya simu ya za mkononi Tigo alifariki dunia baada ya kile kinachosemekana kuwa alikunywa pombe nyingi.
 
Walioshuhudia tukio hilo walisema awali marehemu alikuwa anakunywa pombe na wenzake katika  bwaro la polisi  mjini Shinyanga lakini baadaye mwenzao alizidiwa na kulazimika kumrudisha nyumbani kwake ili akapumzike na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ndipo wakampeleka katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu lakini akafia njiani.
 
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kabla ya kifo hicho marehemu alikuwa anashindana na wenzake kunywa pombe lakini pombe zilimshinda na kuzidiwa hadi kupelekea kifo chake.
 
Naye  rafiki wa marehemu John Maganya  alisema ameshtushwa na taarifa za kifo cha rafiki yake kwani enzi za uhai wake marehemu alikuwa ni mzoefu wa kunywa pombe na wakati mwingine akilewa alikuwa anazimia na akizinduka anaendelea na shughuli zake kama kawaida lakini siku hiyo hali ikawa tofauti.
 
“Kifo cha rafiki yetu God Shaini, kimenishtua sana kwani kama ni kunywa pombe alikuwa ni mzoefu na huwa akinywa anazimia na kuzinduka,nadhani pombe aina ya konyagi aliyokuwa anakunywa na wenzake inaweza kuwa chanzo cha kifo chake,kwani alikunywa mizinga mitano ya konyagi”,alisema Maganya.
 
Akielezea tukio hilo diwani wa kata ya Ngokolo mjini Shinyanga Sebastian Peter alisema  kabla ya kifo chake marehemu alikuwa analalamika kusumbuliwa na vichomi tangu asubuhi siku hiyo lakini na baadaye mida ya saa moja jioni akapewa taarifa na wanachi wake kuwa God Shaini  ambaye alikuwa mtunza stoo wa Tigo amefariki kutokana na kunywa pombe kupita kiasi.
 
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dkt Fredrick Mlekwa alikiri kuupokea mwili  God Shaini ,ambaye alikuwa mfanyakazi wa  kampuni ya simu ya Tigo mjini Shinyanga, muda wa saa moja jioni Desemba 25 mwaka huu,akiwa tayari amefariki dunia na mwili wake kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
 
Aliongeza kuwa kutokana na siku hiyo kuwa ni siku ya sikukuu walitegemea pengine tarehe 27 Desemba wangefanya upasuaji wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo hicho lakini ndugu wa marehemu walifika Desemba 26 asubuhi na kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi hivyo kushindwa kufanya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Evarist Mangala alisema hajapata taarifa za kifo cha mtu huyo na kwamba ndugu wa marehemu hawajafika kituo cha polisi kutoa taarifa kuhusu kifo cha ndugu yao .
 
Tayari mwili wa marehemu God Shaini umesafirishwa kwa ajili ya mazishi hapo kesho Siku ya Jumamosi Desemba 28 nyumbani kwa mama yake  Mabatini mkoani Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages