Wawakilishi wa Kudumu kutoka nchi 193 wanaoziwakilisha nchi zao katika
Umoja wa Mataifa, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki
Moon wakati alipolizungumza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya
Ijumaa. Alitumia fursa hiyo, kuainisha vipaumbele vyake vya mwaka
2014, mafanikio na changamoto zinazoukabili Umoja wa Mataifa ikiwamo
migogoro inayoendelea huko Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati
na kwingineko Duniani. Akatahadharisha kwamba kama Jumuiya ya
Kimataifa haitakuwa makini kuna hatari kubwa ya kutokea mauaji
makubwa ya raia kama ambavyo imeshawahi kutokea huko nyuma
Na Mwandishi Maalum, NewYork
Kufuatia machafuko na migogoro inayoendelea katika nchi za Sudani ya Kusini, Afrika ya Kati, Mali na maeneo mengine duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwa makini na kuchukua tahadhari ya juu.
Amesema kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika maeneo hayo jambo analosema hali ikiendelea kama ilivyo sasa kuna hatari kubwa ya kutokea mauaji makubwa ya raia kama ambavyo dunia imeshuhudia katika miaka iliyopita.
Ban Ki Moon, ametoa tahadhari hiyo, mwishoni mwa wiki, wakati alipolizunguza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa . Ambapo alitumia fursa hiyo kuainisha malengo na vipaumbele vyake na Umoja wa Mataifa kwa ujumla kwa mwaka huu wa 2014.
“Kuna mambo ambayo tunapashwa kuwa makini nayo na kuchukua tahadhari kubwa, mgogoro unaoendelea katika Sudan ya Kusini umefikia kuwango cha kutisha. Kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu “ akasema Ban Ki Moon.
Na kuongeza kwamba kufuatia mgogoro huo Umoja wa Mataifa ulifungua milango ya Kambi ya Kulinda Amani katika Sudan ya Kusini ( UNMISS) na kuwahifadhi maelfu ya raia waliokuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha yao.
“ Wengi wao leo hii wako hai ni kwasababu tu, waliwahi kukimbia kwa wakati na kufika kwenye makambi yetu. Tunajitahidi kadri tuwezavyo pamoja na uwezo wetu mdogo kuwa hudumia, lakini hali ni mbaya na mazingira ni ya kutisha” akasisitiza.
Pamoja na kuendelea na jukumu la utoaji wa misaada kwa raia ambao wameyakimbia makazi yao, Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa anaeleza kwamba, jitihada za kutafutu suluhu ya kisiasa kwa mgogogo huo inaendelea.
Akatumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa nchi za IGAD ( Intergovernmental Authority for Development ) na Umoja wa Afrika ( AU) kwa juhudi zao za kusimamia mazungumzo ya kutafuta suluhu.
Aidha katibu Mkuu amezitaka pande zinazohusika kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazugumzo na kuonya kwamba Ofisi ya Kamishna ya Haki za Bindamu inafuatilia kwa karibu sana kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo .
Kwa upande wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, ameelezea wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa mambo unavyoendelea yakiwamo mauaji holela ya raia.
Akazishukuru nchi zinazounda Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati ( ECCAS) pamoja na Ufarasa kwa juhudi zao za kuwasaidia raia wa nchi hiyo pamoja na kurejesha hali ya amani na utulivu. Nakuonya kwamba wale wote wanaouhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu lazima watawajibishwa.
Kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) Katibu Mkuu ameeleza kuwa uwepo wa Brigedi Maalum ( FIB) katika eneo la Mashariki ya Nchi hiyo, kumesaidia sana katika kuweka sawa mambo ikiwa ni pamoja na kupunguza kujirudia kwa machafuko ya mara kwa mara.
Akasisitiza kwamba Jumuiya ya Kimataifa inapashwa kutumia hali ya utulivu iliyopo hivi sasa katika eneo hilo, kutekeleza Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa kuhusu siasa, amani na maendeleo katika DRC na Maziwa Makuu.
Pamoja na kuzungumza migogoro inayoendelea katika baadhi ya nchi za Afrika, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alielezea wasi wasi wake kuhusu sintofahamu zinazoendelea katika baadhi ya nchi za Asia na Ulaya hususani muendelezo wa chuki na uhasama kwa kimsingi ya tofauti za dini, na ukabila.
Akagusia pia migogoro inayoendelea katika Mashariki ya Kati hususani katika nchi za Syria, Misri na mgogoro kati ya Israel na Palestina.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Ban Ki Moon, amesema Umoja wa Mataifa, haupashwi kuziomba au kuzibembeleza nchi wanachama pale unapohitaji kupatiwa wanajeshi, polisi au vifaa wakati ambapo raia wasiokuwa na hatia wakiendelea kuteseka na kupoteza maisha.
Akasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa ni chombo muhimu ambapo maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika lakini akasema anatiwa shaka na baadhi ya misimamo ya viongozi au nchi zenye ushawishi mkubwa.
Pamoja na kuelezea matatizo ya kisiasa na kiusalama na changamoto zake, pia aliainisha baadhi ya mafanikio ya chombo hicho katika mwaka uliopita na kazi kubwa iliyombele yake na hasa likiwamo jukumu ya utayarishaji wa malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.
Your Ad Spot
Jan 20, 2014
Home
Unlabelled
MGOGORO WA SUDAN YA KUSINI UNATISHA-BAN KI MOON
MGOGORO WA SUDAN YA KUSINI UNATISHA-BAN KI MOON
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269