Breaking News

Your Ad Spot

Jan 18, 2014

MWENYEKITI WA CCM, RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA KADA WA SIKU NYINGI WA CCM

RAIS JAKAYA KIKWETE
IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu, Abdulrahaman Kinana kufuatia kifo cha Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali hapa nchini, Ndugu Deusdedith Makandila Mtambalike aliyefariki dunia tarehe 16 Januari, 2014 nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Enzi za Uhai wake, Marehemu Deusdedith Mtambalike, licha ya kuwa Kada hodari wa CCM, aliwahi kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya za Ngara na Muleba Mkoani Kagera, Wilaya ya Igunga katika Mkoa wa Tabora, Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Iringa na katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.

Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Deusdedith Makandila Mtambalike, Kada makini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mmoja wa Viongozi makini katika Utumishi wa Umma aliyewahi kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali hapa nchini”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi zilizosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo.

Taarifa imesema, Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Desudedith Mtambalike, enzi za uhai wake, kama Kada Hodari, Mwaminifu na Mchapakazi wa Chama Cha Mapinduzi, na mmoja wa Wakuu wa Wilaya aliyekuwa makini katika kazi zake ambaye aliutumikia wadhifa huo kwa umakini na uaminifu mkubwa, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Wananchi katika sehemu zote alizofanya kazi.

“Kuondoka kwa Mheshimiwa Deusdedith Mtambalike ni pigo kubwa kwa Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako mchango wa mawazo na ushauri wa Marehemu ulikuwa bado unahitajika sana kwetu sote”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana Salamu zangu za Rambirambi kutokana na kifo cha Kada huyu wa CCM, na kupitia kwako kwa Wanachama na wapenzi wote wa Chama Cha mapinduzi kwa kuondokewa na mwenzao, Bwana Deusdedith Makandila Mtambalike”, amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete amemuomba Mheshimiwa Kinana kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Mtambalike kwa kuondokewa na Baba, Kiongozi na Mhimili wa Familia. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao, huku akiwahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.

Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi, Roho ya Marehemu Deusdedith Makandila Mtambalike, Amina.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages