Breaking News

Your Ad Spot

Jan 23, 2014

NAPE: MAWAZIRI TULIWANYOOSHEA VIDOLE ILI HATUA MADHUBUTI ZICHUKULIWE KUREKEBISHA MAPUNGUFU YANAYOLALAMIKIWA NA WANANCHI, SIYO KUFUKUZWA TU.

NAPE NNAUYE
NA BASHIR NKOROMO
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema hatua ya CCM kuwanyooshea vidole baadhi ya mawaziri ambao utendaji wao ulilalamikiwa na wananchi pamoja na wabunge, haikuwa kutaka watimuliwe tu, bali zichukuliwe hatua madhubuti kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza dhidi mawaziri hao.

"CCM inatambua kuwa hatua ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri hao ingeweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo, lakini hatua hiyo sio njia pekee hivyo hatua ya kuwabakiza kwenye nafasi zao za uwaziri isitafsiriwe kwamba hakuna hatua zozote zilizochukuliwa", alisema, Nape wakati akizungumza leo na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Nape alisema hayo akitoa msimamo wa CCM, kufuatia hivi karibuni Rais Kikwete kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi na wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa mkono na CCM na kufuatia malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo.

Kufuatia uteuzi huo wa Rais Kikwete umeibuka mjadala mkubwa wananachi karibu nchini kote wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri hao.

"Kwanza haikua hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali", alisema Nape.

Nape alisema, CCM hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri na kwamba wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM na CCM haitavumilia usaliti huo akisema kukaa kimya kwa CCM itakua ni kujinyonga yenyewe jambo ambalo chama hakitutaruhusu kabisa.

"Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa wakali sana kwenye mapungufu, kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe", amesema Nape.

Nape alisema CCM itatumiavizuri wingi wa wabunge wake bungeni na wingi wa madiwani wake kwenye Halmashauri kuisimamia vizuri serikali na kwamba kuanzia sasa kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.

"Tunawaomba watanzania kwa ujumla tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu", alisema Nape.

Alisema CCM inawatakia mawaziri hao kila lakheri kwenye kutimiza wajibu wao ina matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa serikali yao.

Mapema Nape akizungumzia ziara za Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti katika mikoa mbalimbali, Nape alisema ziara hizo ni kutokana na maamuzi ya vikao vya ngazi ya juu vya Chama, na kwamba ziara hizo zimeonyesha kuzaa matunda kwa kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.

"Mara baada ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani kukutana na wananchi kusikiliza kero zao, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma", alisema Nape.

Nappe alisema, msingi wa kwanza wa ziara hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu kabisa cha Chama na wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu wa kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.

"Na bila shaka wote tumeshuhudia jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha kuongeza imani ya wananchi kwa CCM. Tumeshuhudia makundi mbalimbali ndani ya jamii yakija kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi hasa walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa CCM", alifafanua Nape.

Nape alisema katika mwendelezo wa ziara hizo mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti walifanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na mambo mengine wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa baadhi ya mawaziri wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara zao.

"CCM kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013. Utaratibu wa watendaji wa serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya", Napa amezidi kufafanua.

Nape alisema baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi bora ya kuondoa mapungufu tuliyoyaeleza.

"Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya habari baada ya kikao hicho tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri husika isipokuwa wanaweza kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na mabadiliko katika kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi" alisema Nape.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages