.Ni kutokana na msimamo wake dhidhi ya wakiuka maadili katika CCM
WAKATI Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekamilisha kazi
ya kuwahoji baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotajwa kuanza mbio za kusaka urais
2015, kabla ya muda, zimeanza kuvuja fununu za najama za kusukwa hujuma dhidi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana na Makamu
Mwenyekiti, Philip Mangula.
Hujuma hizo ni kutoka kwa moja ya makundi ya mitandao ya wasaka urais,
ambayo mgombea wao mtarajiwa ni kati ya waliohojiwa kwa muda mrefu kuanza
kampeni mapema.
Waliohojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM ni;
Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani,
Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu Steven
Wassira na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Januari Makamba na
Mbunge wa Sengerema William Ngereja.
Hujuma dhidi ya Kinana zinakwenda mbali zaidi huku wasiwasi ukitanda
huenda hadi hujuma hizo kuweza kufanikiwa, Kinana atakuwa amelipa gharama kubwa
na hatima yake inaweza kuwa kitendawili kizito siku za baadaye.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka kambi inayotajwa kuhusika na
hujuma hizo kinaeleza kwamba kinachomponza Kinana ni ujasiri usiotarajiwa
alioonyesha kiasi cha kumudu kumshawishi Rais Jakaya Kikwete, kuridhia
awahoji 'wagombea urais', ikielezwa kwamba ujasiri wa Kikwete binafsi si wa
kiwango hicho hususan kwa wanasiasa wanaotajwa kuwa rafiki zake.
“Kuna mambo kadhaa yanayomponza Kinana kwa sasa na kwa kweli
amekwishatambuliwa rasmi adui wa kambi mojawapo ya urais. Tangu achukue nafasi
ya Katibu Mkuu amekuwa akifanya ziara za kujenga chama mikoani, ziara hizi
zimepokewa vizuri kiasi cha si tu kumjenga Kinana kisiasa lakini kukwamua haiba
ya chama iliyofifia. Kwa hiyo, Kinana sasa anakuwa kiongozi mwenye ushawishi
zaidi si tu CCM bali hata katika kada mbalimbali za kijamii, kuanzia wasomi
hadi viongozi wa dini.
“Pili, hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kwenye
maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa Chama, Mjini Mbeya, kwa sehemu kubwa alimsifu Kinana.
Huu ni uthibitisho mwingine kwamba nguvu za Kinana katika CCM ni kubwa sasa.
Lakini kubwa zaidi linalomponza na mbali ni la tatu ni kukataa kuwa na bei,
hanunuliki wala kuhongwa na hapa kundi fulani la urais kwa sababu linaamini
katika nguvu ya fedha, Kinana ni kikwazo kikubwa mno kwao,” kilieleza chanzo
hicho cha habari.
Ni kutokana na hayo, chanzo chetu cha habari kinadokeza mambo matatu
yanayoweza kutekelezwa na kundi hilo dhidi ya Kinana na Mangula, ambao
ushawishi wa nguvu ya fedha kwao ni sawa na kile chanzo cha habari kimeita
“upuuzi”.
Mpango namba moja
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mpango namba moja ni kuunganisha
nguvu kwa mawaziri walioitwa mizigo. Mawaziri hao wanapangwa kujitokeza
hadharani ili kumkabili Kinana, wakimlaumu katika mwelekeo wa kumjengea chuki
dhidi ya wanaCCM, kwamba amewadhalilisha bila kujali kuitwa kwao mizigo msingi
wake ni hoja za wananchi waliokutana na akina Kinana katika mikutano ya
hadhara.
Mpango namba mbili
Mpango namba mbili unatajwa kuwashirikisha baadhi ya wanasiasa wa
upinzani, ukilenga kutengeneza kashfa kwa gharama yoyote ile na wanasiasa hao
wa upinzani wazungumze mara kwa mara hadharani ili kumvunja kasi Kinana. Tayari
mwanasiasa mmoja ambaye ni mbunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Chadema) anatajwa kuhongwa mamilioni ili kutekeleza mpango huu.
Mpango namba tatu
Mpango namba tatu unatajwa kuwa ni wenye gharama kubwa zaidi kwa
Kinana. Mpango huu (hatuwezi kuutaja hapa) kama ukitekelezwa dhidi ya Kinana na
wahusika wakakamatwa na kufikishwa mahakamani basi, adhabu au hukumu dhidi yao
ni kunyongwa.
“Kwa hali ilivyo, kwao Kinana ndiye sasa mwenye ushawishi mkubwa kuhusu
nani mgombea bora wa urais kupitia CCM 2015 na kwa vyovyote vile, wanashindwa
kumshawishi kwa nguvu ya pesa. Amekuwa Katibu Mkuu mwenye ujasiri unaowatia
shaka katika malengo yao kisiasa,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Kikao cha Maadili
Kuhusu kikao cha kamati ya maadili, inaelezwa kwamba baadhi ya wagombea
urais wamekuwa na hofu ya kuchafuliwa katika safari yao kuelekea Ikulu 2015.
“Kinachowatia hofu ni kwamba kamati ya maadili adhabu yake haikatiwi
rufaa. Kwa mfano, mtu akipewa adhabu ya onyo tayari ni doa kwake, akipewa onyo
kali anafungiwa kugombea nafasi ya uongozi kwa miezi sita. Akipewa karipio
anafungiwa kugombea kwa miezi 12 na akipewa dhabu ya karipio kali anafungiwa
kugombea uongozi kwa miezi 18, hii inawatia hofu sana na wanaamini Kinana na
Mangula ni tatizo kwao,” alisema mtoa habari wetu.
Kinana binafsi hakuweza kupatikana kuzungumzia hujuma zinazopangwa
dhidi yake. Na kwa upande mwingine juhudi za kuwapata wahusika wa mpango huo
hazijazaa matunda hadi sasa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kati ya wanaCCM waliowahi kupewa adhabu
ya karipio kali kutokana na utovu wa maadili ni mwanasiasa Thomas Nyimbo,
ambaye alifungiwa kugombea uongozi kwa miezi 18. ©2014 theNkoromo Blog
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269