Breaking News

Your Ad Spot

Feb 7, 2014

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AKUTANA NA BALOZI MPYA WA OMAN NCHINI TANZANIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na  Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania, Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Feb 7. Picha na OMR

TAARIFA RASMI
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKUTANA NA BALOZI WA OMAN NCHINI
Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amempokea Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania Balozi Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kufanya naye mazungumzo. Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Makamu wa Rais amemhakikishia Balozi Ruqaishi kuwa Tanzania na Oman zina uhusiano wa kindugu wa siku nyingi na kwamba uhusiano huo umekuwa ukinufaisha nchi hizi kwa miaka kadhaa. 

Mheshimiwa Makamu wa Rais aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania kwa sasa inashirikiana na Oman kiuchumi na kwamba kuna wawekezaji wengi kutoka Oman ambao wako nchini, sambamba na wengine wanaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Ruqaishi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Oman inafurahia uhusiano wake na Tanzania na kwamba jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unadumu na kunufaisha nchi hizi mbili. Pili alifafanua kuwa, atahakikisha katika kipindi chake cha Ubalozi hapa Tanzania anasaidia kutanua fursa za uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Oman sambamba na kuwafungulia fursa kama hizo wawekezaji walio na nia ya kuwekeza nchini Tanzania. 

Oman licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania na hasa Visiwani Zanzibar, inabakia kuwa ndiyo nchi pekee duniani nje ya Afrika iliyo na wazungumzaji wengi wa lugha ya Kiswahili. Katika siku za hivi karibuni, wawekezaji kutoka Oman wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi sambamba na kuliimarisha shirika la Ndege Tanzania ili limudu ushindani na kuongeza ufanisi wa shughuli zake katika biashara ya safari za anga.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam, Ijumaa Februari 07, 2014

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages