*Asema CCM haijatelekeza wasanii
*Asema nyimbo za Bongo Fleva hazidumu kwa sababu ya mashairi ya kulipua
*Ni kwa sababu ya wasanii kutaka 'watoke' haraka
*Akunwa na Kina Mwana FA, Lina na Lady Jay Dee
NAPE NNAUYE |
KATIBU wa NEC Itikadi na Uenezi-CCM Nape Nnauye amesema, ndoto aliyokuwa nayo ya kazi ambayo angependa kufanya alipokuwa hajawa mwanasiasa ni kuwa askari ambaye ni rubani wa ndege za jeshi.
Amesema maandalizi ya kutimiza ndoto hiyo alikuwa ameianza kwa kuweka kipaumbele kwenye masomo ya fani hiyo ikiwemo fizikia na jiografia wakati anamaliza kidato cha nne.
Nape mwenye umri wa miaka 37, sawa na umri wa CCM, amesema hayo leo alasiri alipododoswa na watangazaji kwenye kipindi cha 'Power Jam' katika Kituo cha Radio cha East Africa, kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambao walitaka awaambie wasikilizaji ni kazi ya fani ipi aliyokuwa akiipenda kuifanya asingekuwa mwanasiasa.
"Kazi niliyoipenda zaidi ni kuwa Mwanajeshi, tena Mwanajeshi mwenyewe rubani wa kurusha ndege za kijeshi...Na hata nilipokuwa namaliza kidacho cha nne, nilikuwa nimejiandaa zaidi katika masomo ya fani hiyo ikiwemo fizikia na jiografia", alisema, Nape.
ANAVYOJITOFAUTISHA NA WANASIASA WALIOPO VYAMA VYA UPINZANI
Akizungumzia tofauti iliyopo kati yake na wanasiasa walipo kwenye vyama vya upinzani kama walivyotaka kujua watangazaji hao, Nape alisema, tofauti kubwa iliyopo ni kwamba yeye ni mwanasiasa ndiyo sababu yupo kwenye chama cha CCM ambacho ni cha siasa lakini wapinzani siyo wanasiasa bali ni wana harakati kwa sababu wapo kwenye vyama vya harakati siyo vya siasa.
"Unajua mimi ni mwanasiasa ndiyo sababu nipo kwenye Chama Cha Mapinduzi ambacho ni chama cha siasa, lakini hao wengine ni wana harakati ndiyo sababu wapo kwenye vyama vya harakati. Na hii ndiyo tofauti kubwa ya mimi na wao", alisema Nape.
JE CCM IMEWATELEKEZA WASANII AMBAO HUWATUMIA KWENYE SHUGHULI ZAKE WA KAMPENI?
Akijibu swali la watangazaji hao ambao kwa bahati mbaya mtandao huu haukuweza kuyashika majina yao, ambao walitaka kujua Nape alikuwa anasemaje kuhusu tetesi za mitaani kwamba wasanii CCM imewatelekeza wasanii ambao wamekuwa wakitumia kwenye kampeni zake, Nape alisema si kweli kwamba CCM imewatelekeza.
"Wanaosema kwamba wasanii hao CCM imewatelekeza wanakosea, nadhani kwa kutojua hasa kuwa Chama kinawatumiaje.. Ni kwamba wakati wa shughukli zetu kama za kampeni huwa tunaingia nao mkataba wa kutufanyia kazi na tukisha walipa kwa makubaliano ya kazi husika, kazi ikimalizika hatuwezi kuendelea nao, matarajio yetu ni kwamba wataendelea na shughuli zao kama kawaida", alisema Nape na kuongeza;
"Mikataba ambayo CCM huingia na wasanii ni sawa na ile ambayo tunaingia na Media (vyombo vya habari) kutufanyia shughuli zetu, tukisha walipa huwa ndiyo basi mpaka tunapowahitaji tena.. Lakini Wasanii wanakuwa kwenye shughuli zetu moja ya faida wanazopata ni kupata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili katika kazi zao".
Nape alisema, moja ya matokeo ya wasanii hao kuambatana na Mgombea Urais wa CCM ambaye sasa ni Rais Jakaya Kikwete, kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, ni kupiganiwa kwa hakimiliki za kazi zao hali ambayo alisema, ni utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete ingawa utekelezaji wake bado haujakidhi kiwango.
Nape aliitaka serikali kuweka taratibu endelevu za kuhakikisha utekelezaji wa kupambana na wezi wa kazi za wasanii unakuwa wenye kuonyesha matunda ya uhakika kuliko ilivyo sasa, ambapo licha ya mapambano kuwepo lakini bado wizi nao wa kazi za wasanii upo.
"Moja ya njia ambayo ingewakomboa wasanii, na wakati huo huo ikasaidia kukuza pato la taifa kutokana na kazi zao ni kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake kulingana na kazi aliyofanya. Ikumbukwe kwamba ukimwezesha msanii kuwekeza katika kazi zake kama muziki naye atachangia kuinua uchumi wa taifa kwa kulipa kodi", alisema Nape.
Nape aliwapongeza wasanii hasa wa muziki wa Bongofleva, kwa kuisaidia CCM katika kampeni zake za kuska kuongoza nchi na hatimaye kushinda, na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo hawakukosea kwa sababu CCM ndicho chama makini chenye mwelekeo wa uhakika na wa kueleweka katika kuwatumikia Watanzania.
KWA NINI NYIMBO NYINGI ZA BONGOFLEVA HAZIWI ENDELEVU?
Akizungumzia hali ya muziki wa wasanii wa Bongofleva, Nape alisema, tatizo kubwa linalosababisha muziki wao kuchuja haraka ni kutokana na kutokuwa na mashairi yenye mashiko na uhalisia hasa katika masuala ya mapenzi ambako wengi wamejikita.
Nape alisema, wakati wanamuziki wa zamani kama kina Mbaraka Mwinshehe waliimba mashairi yenye uhalisia hata katika mapenzi, mashairi ya wanamuziki hawa wa Bongo Fleva hayana uzito huo sababu kubwa inayowapeleka kwenye tungo za mashairi ya kulipua ikiwa ni tamaa ya kutaka mafanikio ya haraka.
"Msanii anakuwa na tamaa ya kutaka atoke haraka, akitoa singo yake moja tu anataka apate kila tu, nyumba nzuri, gari la kifahari na pesa za kujirusha kwenye klabu za starehe, basi", alisema Nape.
WANA-BONGOFLEVA WANAOMKUNA
Akijibu kuhusu wanamuziki gani za muziki wa kizazi kipya anaowaona kuwa ni magwiji katika fani, Nape alisema, ni wengi lakini Kina Mwana FA, Lina na Lady Jay Dee ni miongoni mwa wanamuziki wa muziki wa fani hiyo ambao wanamkuna.
Nape alimaliza kuhojiwa katika kipindi hicho kwa kuimba wimbo wa 'zilipendwa' ambao baadhi ya mashairi yake ni; "Napenda nipate lau nafasi, nipate kusema na we kidogo aa mama aa, mwenzio naumia....
Nape alisema, ni mpenzi wa muziki kiasi kwamba nyumbani kwake na seti za vyombo vya muziki mithili ya Studio na karibu vyombo vyote vya muziki ikiwemo gita, drums, tumba na kinanda anajua kuvicharaza na kwamba kupiga vyombo vya muziki ndiyo ulevi wake mkubwa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269