Zikiwa zimepita wiki chache tangu kufanyika kwa Mkutano uliojadili kwa kina kuhusu ujangili dhidi ya tembo na biashara haramu ya pembe za tembo uliofanyika Jijini London, Uingereza, Jana Jumanne, hapa Jijini New York, Marekani, palifanyika majadiliano mengine yakihusu pia sifa na uzuri wa mnyama tembo na hatari inayomkabili.
Majadiliano hayo na ambayo yaliwavutia washiriki wengi, yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya National Geograpy na ABC na yalifanyika katika jengo lijulikanalo kama ABC HOME lilipo Broadway, jijini New York.
Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alikuwa kati ya wanajopo wanne walioalikwa kushiriki majadaliano hayo ambayo yaliongozwa na Chelsea Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foudantion.
Wanajopo wengine walikuwa ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society, Bw. John Heminway mwandishi na mtengeneza filamu ambaye pamoja na mwanajopo mwingine Bryan Christy wameshiriki katika kutengeneza filamu ijulikanayo kama “The Battle for Elephants” filamu hii inatarajiwa kuonyeshwa february 27 kupitia Channel ya National Geograpy.
Wanajopo hao wakiongozwa na Chelsea Clinton, walipata fursa ya kila mmoja wao kuelezea nini yeyé kama mtu binafsi au kupitia taasisi anayoiwakilisha ametoa mchango gani katika suala zima la uhifadhi wa Tembo na uthibiti wa mauaji holela ya Tembo na biashara haramu ya pembe za tembo.
Balozi Manongi kwa upande wake, alielezea juhudi mbalimbali ambazo serikali inafanya katika kukabiliana na ujangili dhidi ya tembo, pamoja na biashara haramu ya pembe , aidha alielezea dhamira na nia ya serikali ya kuendeleza mapambano ya kuwanusuru tembo kupitia awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza.
Balozi pia alijibu maswali mbalimbali na kutolea ufafanuzi hoja zikiwamo kuhusu kwanini operesheni tokomeza ilisitishwa, na je serikali ilikuwa na mpango gani kuhusu shehena ya pembe za ndovu ambayo iko katika maghala.
Kwa ujumla wanajopo wote walikubaliana kwamba, mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ni vita ngumu hasa ikizingatiwa kwamba mtandao unaohusika na biashara ya pembe za tembo ni mpana sana na unaohusisha watu wengi.
Na kwa sababu hiyo wamehimiza mambo kadhaa yakiwamo, ushiriki wa wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii kitaifa na kimataifa, udhibiti wa soko na hitajio la pembe za ndovu, utoaji wa elimu kwa umma, uwezeshwaji wa watendaji katika ngazi mbalimbali, na uimarishaji wa sheria.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269