Breaking News

Your Ad Spot

Feb 24, 2014

WAZIRI NYALANDU AWANG'OA VIGOGO IDARA YA WANYAMAPORI

Dar es Salaam, Tanzania
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu leo ametangaza kuwang'oa viongogo wa ngazi ya juu katika Idara ya wanyamapori akieleza kuwa ni kutokana na kutoridhishwa na utendaji wao.
Ifuatayo ni Taarifa rasmi ya tamko la Waziri Nyalndu,  kama alivyolisoma leo na theNkoromo Blog kupata nakala ya tamko hilo

Leo, TAREHE 24 Februari, 2014 Natangaza kuubadili uongozi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya maliasili na Utalii kama ifuatavyo:

Ninamuondoa Profesa Alexander Songorwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii.  Nachukua hatua hii kutokana na kutokuridhishwa kwangu na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika mapambano dhidi ya ujangili yanayoendelea nchini.  Aidha, hatua hii ni utekelezaji wa Azimio la Bunge lililotolewa tarehe 22 Disemba, 2013, lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza.

Utekelezaji wa agizo hili unaanza mara moja, nami namteua Bwana Paul Sarakilya kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wziara ya Maliasili na Utalii kuanzia sasa.

Aidha, ninamuondoka Profesa Jafari Kidegesho katika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na kumteua Dr. Charles Mulokozi kuchukua nafasi hiyo.

Hali kadhalika, ninamteua Bwana Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji – Ujangili na anachukua nafasi ya anayeenda kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Vilevile, Bibi Nebbo Mwina anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, na Bwana Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori. Pamoja na Kitengo cha Uzuiaji – Ujangili nilichokitaja awali, hivi ni vitengo vya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utafiti.

Nawaagiza kwamba Wakurugenzi na Wakuu wote wa kila Idara, kila Shirika, na Taasisi zote ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutengeneza viashiria muhimu vya utendaji kazi (Key Performance Indicators) nakukabidhi kwangu ndani ya siku 30 zijazo.  Viashiria hivi ni hatua ya kufanikisha yafuatavyo, 1)  Malengo ya wizara, 2)  Uwajibikaji, 3) Uwazina 4) Ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku.  Ni sharti tutekeleze mikakati ya wizara katika mifumo inayopimika, tuweze kujipima natuweze kupimwa, natutumikie Taifa kwa uadilifu.

Kwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo mimi mwenyewe, Lazaro Nyalandu, atapaswa kuzingatia na kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Mwenendo (Code of Conduct) ambazo zitapendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara.  Baraza hili liwe limeitishwa na Katibu Mkuu wa Wizara kabla ya mwisho ya mwezi ujao.  Azma ya kanuni hizi ni kuwa na misingi bora ya utumishi, uwajibikaji, utu, usawa na haki katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.

 
Mungu ibariki Tanzania.

Asante.
 
Lazaro S. Nyalandu (MB)
Wizara ya Maliasili na Utalii
24/02/2014

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages