Mkurugenzi Mkuu, Idara Kuu ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa
anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya
Takwimu ya Umoja wa Mataifa, akifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi
wa mkutano huo wa wiki moja Unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 24 ambazo ni
Wajumbe wa Kamisheni hiyo. Mkutano wa Kamisheni ulifunguliwa na Bw.
WU HONGBO, Katibu Mkuu Msaidizi anayeongoza Baraza la Umoja wa Mataifa
la Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC) Katika Hotuba yake Bw.
HONGBO ametoa changamoto kwa wataalamu hao wa Takwimu ya kuhakikisha
kwamba wanafuatilia kwa karibu majadiliano yanayoendelea kuhusu ajenda
mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015 kwa kile alichosema,
utekelezaji wa malengo hayo utahitaji kuungwa mkono na takwimu rasmi na
endelevu.
Na Mwandishi Maalum, New Yok
Wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, wamepewa changamoto ya kuhakikisha kwamba, Takwimu rasmi na sahihi zinaunga mkono pamoja na mambo mengine, utekelezaji na usimamizi wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu (SDGs) baada ya 2015.
Changamoto hiyo imetolewa siku ya Jumanne na Katibu Mkuu Msaidizi Bw. WU HONGBO anayeongoza Baraza la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). Bw. HONGBO alikuwa akifungua rasmi mkutano wa wiki moja wa wajumbe wanaounda Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa.
Wajumbe hao ni kutoka nchi 24 ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ujumbe wake katika Mkutano huu unaongozwa na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Idara Kuu ya Taifa ya Takwimu.
Bw. WU HONGBO amewaeleza wataalamu hao wa masuala ya Takwimu kwamba, mwezi wa Tisa mwaka huu, Umoja wa Mataifa, utaandaa mikutano kadhaa ya kilele, ukiwamo Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu maendeleo ya mataifa ya visiwa vidogo.
Ni katika kipindi hicho hicho pia ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaalika Wakuu wa Nchi na Serikali, wafanyabiashara, vyama visivyo ya kiserikali, na watu wa kada mbalimbali kuhudhuria mkutano wa kilele kuhusua masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi.
“ Hivi sasa kuna mchakato unaoendelea wa majadiliano ya wazi ya Kikundi Kazi kuhusu ajenda mpya za Malengo ya Maendeleo Endelevu baada ya 2015 ( SDGs).
Majadiliano haya na mengine , ni wazi kwamba nafasi na mchango wa Takwimu ni muhimu sana katika kuchangia na kutoa mwongozo wa uundaji wa será na uundwaji wa kamati za ufuatiliaji wa utekeleazaji wa makubaliano yatakayofikiwa” akasisitiza Katibu Mkuu Msaidizi
Katika kuhakikisha kwamba, wataalamu hao kutoka Taasisi za Kitaifa za Takwimu wanafuatilia kwa karibu mikutano mbalimbali muhimu inayoendelea katika Umoja wa Mataifa, yakiwamo majadiliano ya Kikosi Kazi kuhusu Maendeleo Endelevu baada ya 2015.
Katibu Mkuu Msaidizi, Bw. HONGBO amesema, wakati mkutano huo wa Kamishieni ya Takwimu ukifanyika, katika ukumbi mwingine, kulikuwa kukiendelea majadiliano ya awamu ya tisa kuhusu maendeleo endelevu baada ya 2015.
“ Wiki hii inatoa fursa ya aina yake kwenu, pamoja na ajenda mbalimbali zinazowakutanisha hapa, na wakati huu mkiendelea na mkutano wenu, kuna mkutano unaoendelea kuhusu maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo.
Itakuwa vema na ni matumaini yangu kuwa mtaitumia fursa hii kuwasiliana na kubadilishana mawazo na wajumbe wenzenu wanaohudhuria mkutano huo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba malengo hayo mapya ya maendeleo endelevu utekelezaji wake unaungwa mkono na Takwimu rasmi na endelevu” akasisitiza.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 30 ambazo ziliteuliwa kushiriki katika majadiliano ya Kikosi Kazi kuhusu maandalizi hayo ya SGDs baada ya 2015.
Katika mzunguko huu wa tisa wa majadiliano wa hayo kuhusu SDGs, Tanzania inawakilishwa na Dkt. Lorah Madete, Afisa Mkuu na mchambuzi wa Sera kutoka Ofisi ya Rais, Kamisheni ya Mipango.
Your Ad Spot
Mar 5, 2014
Home
Unlabelled
TAKWIMU RASMI NA ENDELEVU NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA SERA ZA MAENDELEO -UMOJA WA MATAIFA
TAKWIMU RASMI NA ENDELEVU NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA SERA ZA MAENDELEO -UMOJA WA MATAIFA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269