Meneja
wa Benki ya Exim, Tawi la Temeke Bi Joyce Sinamtwa (wakwanza kushoto)
akiwaelekeza wanafunzi wa Shule ya Msingi Kilakala jinsi ya kutumia
kompyuta mara baada ya kuzindua maabara ya kompyuta iliyowekwa na benki
hiyo katika Shule hiyo iliyopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam
jana. (Picha na mpiga picha wetu).
Meneja
wa Benki ya Exim, Tawi la Temeke Bi Joyce Sinamtwa (wapili kushoto)
akipeana mkono na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilakala Abdul
Kuratasa mara baada ya kuzindua maabara ya kompyuta iliyowekwa na benki
hiyo katika Shule hiyo iliyopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam
jana.
Meneja
wa Benki ya Exim, Tawi la Temeke Bi Joyce Sinamtwa (wapili kushoto)
akikata utepe kuzindua maabara ya kompyuta iliyowekwa na benki hiyo
katika Shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo wilayani Temeke jijini Dar es
Salaam jana. Akishuhudia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilakala
Abdul Kuratasa.
IKIWA ni sehemu ya shughuli zake za kijamii katika kukuza
uwezo wa maendeleo miongoni mwa vijana nchini Tanzania, Benki ya Exim
Tanzania, ambayo inaamini kuwa ugunduzi ni maisha, imekabidhi maabara ya
kompyuta katika Shule ya Msingi Kilakala iliyopo Wilayani Temeke katika
Mkoa wa Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa hafla ya
makabidhiano hayo iliofanyika jana shuleni hapo, Meneja wa Benki ya
Exim Tawi la Temeke, Bi Joyce Sinamtwa alisema kuwa msaada huo wa
maabara ya kompyuta, unadhihirisha jitihada za Benki ya Exim katika
kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania kwa kuwekeza kuwa rasilimali watu
bora katika siku za usoni.
Alisema,
"Mbali na maktaba iliyowekwa mwaka jana, maabara hii ya kompyuta pia
itasaidia kuwaletea maendeleo watoto hawa na kuonyesha dhamira yetu
ya kuwekeza katika viongozi wa baadaye wa taifa hili. Baadhi
ya wanafunzi hawa wana uwezo mkubwa wa kufikiri lakini wanakosa fursa ya
kupata vifaa kama hivi vya kielimu. Benki ya Exim imeamua
kuwajengea uwezo zaidi katika kuwafungulia njia wanafunzi hawa ili
kukabiliana na changamoto za kimaendeleo hapo baadaye.” Bi. Sinamtwa
alisema kuwa uongozi wa benki yake unaamini kwamba kwa kuweka maabara
hiyo ya kompyuta katika shule hiyo, wanafunzi wengi wataweza kutumia
fursa hiyo kuendeleza ujuzi wao na hivyo kuwa wabunifu katika maisha yao
ya kila siku.
Bi Sinamtwa alibainisha
kuwa tangu benki hiyo ilipoichukua shule hiyo na kuwa kama mlezi wake
mnamo Agosti 2012,shule imekuwa ikipiga hatua zaidi kutokana na misaada
mbali mbali iliyotolewa na benki hiyo, ambayo ni pamoja naukarabati wa
miundombinu, kutoa madawati, vitabu na vifaa vingine vya kitaaluma.Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule
ya Msingi Kilakala Bw. Abdul Kuratasa alisema, "Ni dhana nzuri ya
kuwajengea mazingira mazuri watoto kuwa wataalam katika sekta ya sayansi
na teknolojia na kuendana na mabadiliko ya dunia. Sasa nao pia wana
nafasi ya kushindana vilivyo na wanafunzi kutoka shule
binafsi. Tunawashukuru Benki ya Exim kwa uwekezaji huukwa watoto."
Bw. Kuratasa alisema
mradi huo utawaletea watoto hao manufaa makubwa, kuongeza kuwa kabla ya
hapo baadhi ya wanafunzi hawakujua kompyuta inaonekanaje, ila sasa
wamepata maabara ya kompyuta safi kutoka Benki ya Exim.
"Wanafunzi
wa Kilakala kwa kupitia msaada toka kwa walimu na wataalam wa
IT sasa wamepata fursa ya kujifunza kompyuta. Tunashukuru
sana na kujiona kama shule yenye bahati kuwa na mradi huu," alisema.
Akitoa maoni yake juu
ya msaada huo, Mwanafunzi wa Darasa la Sita wa Shule ya Msingi Kilakala
Nasra Abeid alisema,"Hii ni nafasi tuliyokuwa tukiisubiria kwa muda
mrefu. Sasa tunaweza kuwa na uhakika wa kutumia kompyuta kabla ya
kwenda shule ya sekondari, hii imekuwa ndoto ya kweli kwetu. Tunashukuru
sana."
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269