Breaking News

Your Ad Spot

May 13, 2014

HAKUNA NCHI ITAKAYOWEZA KUKABILIANA NA MADHARA YA SILAHA ZA NYUKILIA

Na Mwandishi Maalum, New York
Mkutano wa  Tatu wa maandalizi  ( Prep Com) ya  mkutano  utakaofanyia  mapitio  ya  Mkataba wa Kimataifa Unaozuia Usambaaji Holela wa  Silaha za Nyukilia ( NPT) umemalizika  mwishoni  mwa wiki iliyopita, huku wanachama wakitoka  bila ya kuwa na makubaliano ya pamoja kuhusu mapendekezo  na mpango wa utelelezaji yatakayowasilishwa katika mkutano  huo wa  mapitio  unaotarajiwa kufanyika  mwaka 2015.

Licha ya kwamba nchi hizo hazikutoka na makubaliano  ya pamoja,  jambo la msingi  na ambalo  linakubalika  na wote ni kwamba hakuna nchi au shirika la kimataifa linatakaloweza kukabiliana na madhara ya  mlipuko wa silaha za nyukilia iwe kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Na kwa sababu hiyo nchi 136 zilizochangia hoja ya  madhara ya  silaha za nyukilia kwa binadamu  zilisisitiza kuwa  njia pekee ya kumwepusha mwanadamu na  madhara hayo ni kuondokana  au kuachana kabisa na  silaha za  hizo.
Hata hivyo, nchi  zinazomiliki silaha za nyukilia ambazo ni  Ufaransa,  Marekani, Uingereza, China na Urusi, licha ya kutambua  madhara ya silaha hizo, zenyewe zimependekeza kuwa upunguzaji wa  silaha hizo, ufanyike hatua kwa hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa  mkutano huo uliofanyika kwa wiki mbili  kuanzia  April 28 hadi Mei  Tisa,   Mwenyekiti wa mkutano huo wa Tatu  Mwakilishi wa Kudumu wa Peru katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Enrique Roman – Morey  alieleza kwamba  kutofikiwa kwa makubaliano ya pamoja kuhusu mapendekezo na mpango wa utekelezaji hakukutokana na  kutokuwepo wa utashi wa kisiasa   baina ya wajumbe bali ni ufinyu wa muda zaidi wa majadiliano.

Kwa mujibu wa Balozi Morey nchi  149 kati ya  189 ambazo ni wanachama wa NPT walihudhuria  mkutano huo. Na kwamba nchi  tano zinazomiliki silaha za nyukilia yaani  Marekani,  Urusi,  Uchina, Ufaransa na Marekani, ziliwasilisha taariza zao zinazofanana kuhusu mchakato unaoendelea  wa kupunguza malimbikizo ya silaha hizo.

Mwenye kiti huyo wa  Prep Com alibainsha kwamba nchi wa wanachama wa NPT walijadili  vipengele muhimu  vinayounda NPT ambavyo ni  uzuiaji wa usambaaji holela wa silaha za nyukilia,  upokonyaji wa silaha za nyukilia,  matumizi salama  ya nishati ya nyukilia,  madhara ya  nyukilia kwa mwanadamu na   Uanzishwaji wa Ukanda  huru dhidi ya silaha za nyukilia na silaha zingine za maangamizi katika eneo la Mashariki ya kati.

 Aidha   Balozi  alieleza  pia kwamba jambo  jingine lililojadiliwa kwa mapana na wanachama wa NPT ni kuhusu  haja na umuhimu wa  mataifa kuridhia mkataba wa kimataifa unaozuia majaribio ya silaha za nyukilia (CTBT). Hadi sasa    ni nchi 162 tu ndizo zilizoridhia mkataba huo.

 Jambo la muhimu ambalo  Mwenyekiti wa PrepCom anasema lilionekana  dhahiri katika mkutano huo ni kuwa  nchi zote zilizoshirikia  mkutano huo wa maandalizi,  zimeonyesha uwajibikaji  katika kuhakikisha kuwa Dunia  inaondoka na inakuwa huru dhidi ya silaha za nyukilia.

Mapendekezo na mpango wa utekelezaji uliopitishwa mwishoni mwa mkutano huo, utawasilishwa na  Mwenyekiti wakati wa mkutano wa  mapitio ya NPT utakofanyika mwezi Mei mwaka 2015.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutao huo uliongozwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi   akiwamo   mtaalamu  kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania,  Kanali  Dr. Edward Massala.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages