Wakili
wa kujitegemea wa Baraza la wazee wa kanisa la Moravian Usharika wa
Tabata Bw. Benjamin Mwakambe akiongea na waandishi wa habari kuhusu amri
ya iliyotolewa na mahakama kuzuia Bodi ya wadhamini wa kanisa la
Moravian Kanda ya Kusini kusimamisha huduma za kiroho na kijamii katika
eneo hilo. Wengine ni Mzee Kiongozi wa Usharika huo Bw.Ernest Isakwisa(kulia) na Hamphrey Mgema (kushoto)
Baadhi
ya Wazee wa Kanisa la Moravian usharika wa Tabata wakifuatilia masuala
mbalimbali wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari.
======= ======== ======
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
19/6/2014.Dar es salaam.
Uongozi
wa Baraza la wazee wa Kanisa la Moravian usharika wa Tabata jijini Dar
es salaam umekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari
kuwa huduma za kiroho na kijamii katika ushirika huo zimesimamishwa
kufuatia mgogoro wa uongozi wa usharika huo kupelekwa mahakamani.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kwa niaba ya Baraza la
wazee wa usharika wa Moravian Tabata Mzee Kiongozi, Bw. Humphrey Mgema
amesema kuwa usharika huo ambao uko chini ya jimbo la Mashariki
linaloongozwa na Mwenyekiti,Mchungaji Dkt.Clement Fumbo umekuwa katika
mgogoro wa uongozi kwa zaidi ya miaka 2 na uongozi wa jimbo la Kusini
linaloongozwa na Askofu Lusekelo Mwakafwela.
Amesema
tofauti za uongozi na hasa baraza la wazee wa usharika
huo kutokubaliana na baadhi ya maagizo ya askofu Mwakafwela na Bodi ya
Wadhamini kuhusu umiliki na uangalizi wa usharika huo vimesababisha Bodi
hiyo kwenda mahakamani kuzuia kufanyika kwa shughuli zozote katika eneo
la usharika huo.
“Yapo
mambo mengi ambayo ni kiini cha mgogoro huu lakini jambo kubwa ni hatua
tuliyoichukua ya kutokubaliana na baadhi ya maagizo yake ambayo
yalionekana kutolinufaisha kanisa na hasa madai ya Bodi ya Wadhamini wa
Kanisa la Moravian kanda ya kusini kututaka sisi tutamke wazi kuwa wao
ndio wamiliki halali wa kanisa hilo” Amesema.
Ameeleza
kuwa tamko la maaskofu lililotolewa na mwangalizi wa Kanisa la Moravian
jimbo la Kusini askofu Lusekelo Mwakafwela katika ushirika wa Kinondoni
kuzuia ibada na shughuli za kijamii katika usharika wa kanisa hilo eneo
la Tabata halikubaliki na kuongeza kuwa limeleta athari kwa washirika
wa kanisa hilo zaidi ya 700 na kuwafanya baadhi yao kushindwa kuhudhuria
ibada.
Aidha,amesema kufuatia
mgogoro huo kushindwa kupatiwa ufumbuzi katika ngazi za juu za kanisa
hilo na hatua iliyochukuliwa ya kuwapeleka mahakamani wao kama baraza la
wazee wameamua kuadai haki yao kupitia Wakili wa kujitegemea Bw.
Benjamin Mwakambe.
Amesema
kuwa licha ya baadhi ya mashauri kuendelea kusikilizwa mara mahakama
imetoa Amri kuwa shughuli za ibada na kijamii katika usharika huo
ziendelee kama kawaida.
Kwa
upande wake wakili wa kujitegemea wa Baraza la wazee wa kanisa hilo Bw.
Benjamin Mwakambe amefafanua kuwa hukumu ya mahakama iko wazi na
kuongeza kuwa maombi ya Bodi ya wadhamini yalikataliwa mahakamani.
“Mahakama
imeshaamua katika masuala haya kuwa ile jamii iachwe na wala
isibugudhiwe na mtu yeyote na kama kuna usumbufu wa aina yoyote
utakaofanywa dhidi yao ni wazi watakuwa wamedharau amri ya mahakama”
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269