Breaking News

Your Ad Spot

Jul 25, 2014

BUNGE MAALUM LA KATIBA KUENDELEA: SITTA

Na Winner Abraham na Rose Masaka-
MAELEZO-Dar es salaam

Mwenyekiti  wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa  Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama ulivyopangwa  Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.


Amesema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia  vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.


Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.


 “Kamati hiyo, imeamua  kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba  Bunge Maalum la Katiba liendelee   kwa  sababu  yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuikarabati Tume ya  Taifa ya Uchaguzi(NEC).


 “Mambo mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano,haki za wakulima,wafugaji,wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,”alisema Sitta katika taarifa hiyo.


 Aidha  aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa  zaidi ya theluthi  mbili   ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.


Alisema  hatua ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.


 Aliongeza kwamba Kamati hiyo, inaona  kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira halisi  ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji  kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.


 Alisema Kamati hiyo inarejea kwamba  wajumbe hao  629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.


“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.


 Mwenyekiti huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo,  uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye  inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu  zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.


 Alisema Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.


Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi,walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.


“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti  hadi  asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema  Sitta  katika taarifa yake. 


Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye  kuipigia kura Katiba mpya  ni pamoja na  kupoteza mabilioni ya fedha  za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno  mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages