Breaking News

Your Ad Spot

Jul 25, 2014

FUSO LAUA WAFANYABIASHARA WAWILI, 46 WAJERUHIWA

-Walikuwa wanakwenda mnadani
-Wawili hali zao mahututi
Na Chibura Makorongo, Shinyanga
Watu wawili wamekufa papo hapo na wengine 46 kujeruhiwa baada ya lori aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria na mizigo yao kutoka katika kijiji cha Kiloleli kwenda katika mnada wa Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuacha njia na kupinduka kutokana na kile kilichotajwa kuwa mwendo kasi.

Ajali hiyo imetokea leo saa tatu asubuhi katika kijiji na kata ya Uchunga wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga baada ya lori lenye namba za usajili T680 ARL aina ya Fuso lililokuwa limepakiza mizigo na wafanyabiashara ambao idadi yao bado haijajulikana  likitokea kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu kwenda katika mnada wa Mhunze uliopo Kishapu liliacha njia na kupinduka.

Walioshuhudia ajali hiyo wamesema gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi likamshinda dereva, hivyo kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha amesema katika taarifa za awali zinaonyesha kuwa ajali hiyo imetokana na mwendo kasi wa lori hilo.

Amesema lori hilo aina ya Fuso, mali ya Ngasa Seni, mkazi wa Kiloleli lilikuwa likiendeshwa na Shija Ngasa ambaye pia ni mfanyabiashara, mkazi wa Kiloleli wilayani Kishapu ambaye alitoroka baada ya kutokea ajali hiyo na anatafutwa na jeshi la polisi.

“Lori hili lilikuwa linatoka Kiloleli kwenda Mhunze mnadani,lilikuwa limepakiza abiria wengi wakiwa wafanyabiashara,liliacha njia na kupinduka,chanzo mwendo kasi”,alifafanua kamanda Kamugisha.

“Taarifa za awali tulizonazo watu wawili wamefariki dunia,mmoja anaitwa Difa Shimo(28) mkazi wa Bulima Kishapu, mwingine jina lake bado halijafahamika,majeruhi wako 46, 35 wako katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga, 11 wapo katika Hospitali ya Kolandoto iliyopo katika manispaa ya Shinyanga”,aliongeza Kamugisha.

Kufuatia ajali hiyo kamanda Kamugisha alitoa wito kwa wamiliki wa magari,wananchi wakiwemo wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia magari yasiyo ya abiria kusafiria.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dk. Maguja Daniel amesema wamepokea miili miwili ya marehemu na majeruhi 35 na wanaendelea kuwapatia matibabu huku wawili hali zao zikiwa mbaya.

Ajali hiyo ya Fuso imetokea ikiwa ni siku moja tu baada ya abiria 63 kunusurika kufa baada ya basi la Super najimunisa likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka katika eneo la kijiji cha Usanda kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages