Breaking News

Your Ad Spot

Dec 14, 2014

GWIJI WA MASUALA YA MTANGAMANO JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI AFARIKI DUNIA

Balozi Ndayiziga katika mojawapo ya warsha ya EAC hivi karibuni. Kulia ni mtaalamu wa habari na mratibu wa mafunzo ya wandishi wa habari EAC, Bw. Sukhdev Chhatbar.

Mkufunzi katika Mafunzo hayo, Balozi  Jeremy Ndayiziga (kushoto enzi za uhai wake) akimkabidhi cheti Mroki Mroki, kutoka Father Kidevu Blog ambaye pia ni Mpigapicha wa Masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,  kwa kushiriki kikamilifu mafunzo hayo ya masuala ya Mtengamano wa EAC. Anaeshuhudia Katikati ni Elizabeth Wanyoike wa GIZ ambao walifadhili mafunzo hayo na Jumuia ya Afrika Mashariki.
**********
 Na Mtua Salira, EANA
Mshauri Mtaalamu wa muda mrefu wa Masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Balozi Jeremy Ndayiziga (54) amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi ugonjwa wa kisukari mjini Bujumbura,Burundi.

Balozi huyo raia wa Burundi kwa mujibu wa marafiki wa karibu na ndugu zake alifariki Jumatano wiki iliyopita na anatarajiwa kuzikwa nchini Burundi Jumanne ijayo, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.

Kutokana na hali yake ya afya kuendelea kudorora, Balozi Ndayiziga alilazimika kukatwa mguu wake wa kulia  katika Hopsitali ya Nairobi kutokana kuzidiwa na ugonjwa wa kisukari na hivyo kubaki hospitalini kwa miezi ipatayo minne. Afya yake ilionekana kuimarika kidogo na alikuwa anakaribia kupona.

Mara ya mwisho alionekana makao makuu ya EAC mjini Arusha, Tanzania katikati ya Novemba mwaka huu katika mkutano wa Maofisa Mawasiliano wa EAC.
Jina la Balozi Ndayiziga ni maarufu kwa watendaji wa EAC kutokana na umahiri wake wa uchapaji kazi,uongozi wa busara na kuwa muumini wa itikadi ya Shirikisho la EAC. Ndiye aliyeiongoza nchi yake katika harakati za kujiunga na EAC 2007.

‘’Marehemu Balozi Ndayiziga alikuwa mtu maarufu, mchapakazi mwenzangu na kwa kweli, zaidi ya yote alikuwa rafiki yangu wa karibu sana,’’ alisema Jean Rigi,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki  nchini Burundi na kuongeza kuwa wengi watamkosa na ni pigo kubwa kwa wote wanaopigania kujenga Afrika Mashariki na raia wake.

Mkongwe wa masuala ya habari nchini Tanzania Jenerali Ulimwengu kufuatia taarifa ya kifo hicho alisema: ‘’Nimepata mshtuko mkubwa! Nilijua kwamba alikuwa anaugua lakini nilifikiri kwamba ni jambo la kawaida tu linaloweza kudhibitiwa.Nimesikitishwa sana kwa sababu alikuwa ni mtu makini na mwalimu mwenye uelewa wa hali ya juu na alikuwa mwakilishi mzuri wa masuala ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Nilifanya naye kazi kwa karibu sana kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano.’’

Naye mmoja kati wafanyakazi aliokuwa anafanya nao kazi kwa karibu ni Sukhdev  Chhatbar, Mtaalamu wa Masuala ya Habari, ambaye alielezea kusitishwa na kifo Balozi Ndayiziga.

‘’Tulikuwa tunawasiliana vyema katika uekelezaji wa miradi mbalimbali.Alikuwa mtu maarufu, mwenye msimamo thabiti,mwenye busara na alikuwa tayari kufanya lolote kuimarisha mchakato wa mtangamano wa kikanda,’’ alisema Chhatbar, mwandishi wa habari maarufu aliyekuwa anasafiri na kusimamia miradi ya pamoja ya EAC na marehemu Balozi huyo katika nchi wananchama wa jumuiya.
Marehemu ameacha mjane na watoto wanne.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages